MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata bidhaa za magendo, zilizoingizwa nchini kwa njia ya panya, ambazo zimeipotezea serikali kodi ya Sh bilioni 3.3 huku zikiwa na thamani ya jumla ya Sh bilioni 4.
Aidha, imetaja maeneo korofi yanayotumika kuingiza bidhaa hizo kuwa ni Bagamoyo, Saadani, Mlingotini, Mbegani Juu, Mbweni, Ununio, Kunduchi, Kawe na Msasani.
Maeneo mengine ni Kigamboni, Ufukwe wa Bamba, Kimbiji, Pemba Mnazi, Kibada, Nyamisati, Kisiju, Mkuranga, Ubungo na katikati ya jiji.
Akitoa taarifa hiyo Dar es Salaam juzi, Kaimu Mkurugenzi Elimu kwa Mlipakodi, Diana Masala alisema kuwa bidhaa hizo, zimekamatwa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Zilikamatwa katika msako uliofanywa na Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Idara ya Upelelezi Tanzania.
Alisema kuwa bidhaa hizo zimekamatwa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu kutokana na utaratibu wa kufanya doria na msako kwa pamoja katika maeneo ya mwambao wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
“Bidhaa zilizokamatwa ni majokofu yaliyotumika, luninga, simu za viganjani, kanga, vitenge, chakula na mafuta ya kupikia. Kufanikiwa kukamatwa bidhaa hizi kumetokana na ushirikiano kati ya TRA, Jeshi la Polisi, JWTZ, matumizi ya vifaa vya kielekroniki na taarifa kutoka kwa wasamaria wema,” alisema Masala.
Alisisitiza kuwa bidhaa za magendo, zinaathiri uchumi wa Taifa kwa ujumla na kwamba wataendelea kudhibiti bidhaa za magendo kwa kufanya doria nchi kavu na bandarini pamoja na misako ya kushtukiza katika maeneo hayo korofi.
Pia aliongeza, watawatoza faini na kuwafutia leseni za biashara Mawakala wa Forodha wanaojihusisha na vitendo viovu na kutoa semina kuhusu madhara na athari za bidhaa hizo.
“Tunawaomba wananchi wa maeneo hayo mtoe taarifa za shughuli za bidhaa bandia zinazofanywa kwa kupiga simu namba 0789 338 930 itarahisisha ukamataji wa bidhaa hizo,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, imekusanya Sh milioni 565.4 kupitia tozo mbalimbali za makosa ya usalama barabarani. Kamishna wa Polisi Kanda hiyo, Simon Sirro alisema kuwa makusanyo hayo ni kwa kupindi cha kuanzia Dsemba 22 mwaka huu hadi Desemba 30 mwaka huu.
‘’Idadi ya magari yaliyokamatwa ni 17,645, bodaboda 1,406 na daladala 6,213 ambapo jumla ya makosa yaliyokamatwa ni 18,849,’’ alisema Sirro.
Pia aliwataka madereva hao kuwa makini kwa kuepuka ajali zisizo za lazima. Aliagiza askari wa usalama barabarani kuhakikisha kuwa watakaobainika wanakiuka sheria hizo wanachukuliwa hatua kali ikiwemo kupelekwa mahakamani na kutozwa faini.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment