DAR ES SALAAM: Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara zitakuwa zikifanyika mjini Dodoma kuanzia mwaka 2017 badala ya Jijini Dar es Salaam kama ilivyozoeleka.
Uamuzi huo umetangazwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. John
Magufuli, wakati akitoa salamu zake za maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru
wa Tanzania Bara, kwenye sherehe zilizofanyika leo katika uwanja wa
Uhuru dar es Salaam.
Katika
salamu hizo, Rais Magufuli ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi, ameeleza
sababu za kufuta sherehe hizo mwaka jana na kuruhusu mwaka huu
zifanyike ambapo amesema sababu moja wapo iliyomfanya afute sherehe hizo
mwaka jana ni kubana matumizi.
“Mwaka
jana nilipouliza gharama za sherehe zile nikaambiwa ni shilingi bilioni
4, nikashangaa, bilioni 4 zote ni za nini?” Amesema Rais Magufuli.
Kuhusu sababu za kuruhusu mwaka huu sherehe hizo zifanyike, Rais
Magufuli ametaja sababu mbili ambazo ni pamoja na kutumia gharama ndogo
huku sababu ya pili akiitaja kuwa ni kutokana na kwamba hizi ni sherehe
za mwisho za Uhuru kufanyika Jijini Dar es Salaam huku akieleza kuwa
kuanzia mwaka 2017, sherehe hizo zitakuwa zikifanyika katika makao makuu
ya nchi Dodoma.
Rais Magufuli pia ametumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio ya
Tanzania katika miaka yake 55 ya Uhuru, huku akieleza mikakati ya
serikali yake ya awamu ya tano katika kuifikisha nchi kwenye kipato cha
kati na kuwashukuru viongozi wakuu wa awamu zilizopita.
Mbali na hayo, Rais Magufuli pia
ameitaja rushwa kama changamoto sugu ambayo bado inaendelea kulitafuna
taifa la Tanzania katika miaka yake 55 ya Uhuru. Vikwazo vingine amesema
kuwa ni tatizo la ajira pamoja na umasikini.
Akizungumza
katika hotuba yake ya shukrani katika maadhimisho hayo ambayo
yamefanyika katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam, Dkt. Magufuli,
amesema kuwa serikali yake itaendelea kupambana na vitendo na rushwa na
ufisadi, kwa ajili ya kuliletea taifa maendeleo.
Aidha
Rais Dkt. Magufuli amesema kuwa serikali itahikisha kuwa inaondoa
uonevu hasa kwa wananchi wanyonge ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto
zinazowakabili ili kila mtanzania aweze kufaidika na matunda ya nchi
yake.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment