Kama nilivyosema katika siku zilizopita
kwamba hakuna mtu ambaye anaweza kufanikiwa pasipo kupambana. Ili ufike
pale ambapo mabilionea wengine walipo kwa sasa, huna budi kupambana na
kujitoa sana katika kila kitu ukifanyacho.
Nimewazungumzia watu wengi, mabilionea
ambao waliweka wazi ni kwa namna gani mtu anaweza akafanikiwa kama
walivyokuwa wao. Kwa leo, tutafahamu mambo mbalimbali kuhusu bilionea
namba moja Afrika, Mnigeria, Aliko Dangote.
Mwaka huu, serikali ya Tanzania ilimpa
ruhusa kutengeneza kiwanda cha kutengeneza saruji nchini hapa. Hicho si
kiwanda chake cha kwanza, ana viwanda vingi ikiwemo Afrika Kusini, Togo,
Nigeria na nchi nyingine.
Amekuwa akiamini sana katika saruji na
mafuta kwa sababu ndivyo vitu ambavyo watu huvitumia kwa wingi. Ni
lazima watu wawe wanajenga kila siku lakini pia, kwa wenye magari ni
lazima wawe wanayaendesha kila siku na ndiyo maana anaamini kwamba
katika vitu hivyo ni lazima ataingiza pesa nyingi.
Dangote ni nani?
Huyu ni bilionea namba moja Afrika ambaye alizaliwa mwaka 1957 na baba yake aliyekuwa bilionea kipindi hicho nchini Nigeria, Mohammedi Dangote na mama yake, Hajia Mariya Sanusi Dantata.
Alianza biashara shule ya msingi
Dangote
anasema kuwa wakati alipokuwa akisoma shule ya msingi alikuwa akifanya
biashara ya kuuza pipi kwa wanafunzi wenzake. Anasema “Nakumbuka
nilipokuwa shule ya msingi, nilikuwa nakwenda kununua mifuko ya pipi na
kuwauzia wanafunzi wenzangu shuleni kwa ajili ya kutengeneza pesa
zangu.”
Aanzisha kampuni yake
Baada ya kumaliza masomo yake ya biashara katika Chuo Kikuu cha Cairo nchini Misri, Dangote akaanzisha kampuni yake aliyoiita Dangote Group huku akiwa na miaka 21 tu.
Huwa hazimi simu siku nzima
Dangote
anasema kwamba kila siku amekuwa mtu wa kufanya kazi. Yupo radhi
kukesha huku akifanya kazi mpaka pale anapokamilisha kile anachokifanya.
Husema kwamba watu wengi wamekuwa wakifanya makosa katika matumizi ya
simu. Huwa hazimi simu yake kwa sababu anaamini hicho ndicho kitu
kinachomfanya kuwasiliana na wafanyabiashara wenzake. Kwa kawaida huanza
kufanya kazi ofisini kwake kuanzia saa kumi na moja alfajiri.
Dangote
anatumia simu iitwayo Nokia Vertu Signature ambayo huuzwa kwa dola
5000-7500 (zaidi ya milioni 10 mpaka milioni 15) ambayo muonekano wake
hufanana na ‘Nokia ya Tochi’
Ni mtu anayesaidia masikini
Mwenyewe huamini kwamba kile alichokuwa
nacho si kwamba Mungu aliamua kumpa kwa ajili yake tu, alimpa kwa sababu
alitaka kuwaona masikini wengine wakipata kutoka kwake. Kila mwaka
amekuwa akitoa kiasi cha naira milioni kumi (zaidi ya shilingi milioni
70) kwa ajili ya masikini, wanawake na watoto wasiojiweza.
Mwaka 2013 wakati Nigeria ilipokuwa na
uhaba wa mafuta, Dangote akatangaza kwamba angechimba kisima kikubwa cha
mafuta Afrika na kusambaza Afrika nzima. Hilo liliwashangaza watu wengi
lakini akafanikiwa na kisima hicho kikaufanya utajiri wake kuongezeka.
Ni lazima unapotaka kufanikiwa uweke msimamo wako katika biashara ambayo
unaamini itakutoa hapo ulipo.
Mungu alimuepusha kifo mara tatu
Huku utajiri wake ukiwa umeanza kukua,
mwaka 1996 alipata ajali ya ndege. Hiyo ilikuwa ni ya mara ya tatu
ambapo kaka yake, mtoto wa Rais, Sani Abacha walikufa lakini yeye
akanusurika kuonyesha kwamba bado Mungu alikuwa na kazi naye.
Ingawa ni bilionea mkubwa lakini Dangote
si mtu anayejivunia utajiri aliokuwa nao. Huvaa suti za kawaida,
hutembelea magari ya kawaida. Ni mtu ambaye muda mwingi anashinda
ofisini kufanya kazi kwani anaamini kwamba kama unataka biashara zako
zisimame, ni lazima uzisimamie kwa nguvu zote, vinginevyo hutofanikiwa.
Sarakasi zake za mapenzi
Dangote amefanikiwa kuoa mara tatu. Mke
wake wa kwanza alichaguliwa akiwa na miaka 20 ambapo baadaye akamuacha
baada ya kupata mtoto naye aliyeitwa Halima, hivyo akataka kumuoa
msichana aliyeitwa Nafisat Yar’adua aliyekuwa binti wa rais lakini
bahati mbaya kwake msichana huyo akakataa kwa sababu alikuwa na urafiki
mkubwa na Halima.
Baadaye Dangote akamuoa Mariya AD
Muhammad Rufai ila wakaachana baada ya kukaa kipindi kifupi. Baada ya
hapo, hakuna mtu anayeemfahamu mke wa Dangote kutokana na maisha yake
kuwa ya siri sana.
Ila mwaka 2014, watu wakahisi kwamba
msichana mrembo, Sylivia Nduka anatoka na Dangote kwani amekuwa
akionekana mara kwa mara katika ndege binafsi ya Dangote na
kilichowafanya watu kuhisi zaidi ni kwamba kwenye akaunti ya Instagram,
msichana huyo aliweka herufi AD mbele ya jina lake, herufi hizo
zinamaanisha Aliko Dangote.
Utajiri wake sasa
Mpaka sasa hivi, Dangote ana utajiri wa
dola bilioni 12 ambazo ni zaidi ya trilioni 24, utajiri huo umekuwa
ukiongezeka siku hadi siku.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment