Aliyekuwa
mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, amewashukuru wananchi kwa kumpigia kura kwa wingi licha ya
baadhi kumsema vibaya kwa kumwita mgonjwa na kwamba angekufa.
Lowassa
ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alitoa kauli hiyo mjini
Mbinga mkoani Ruvuma ambako chama hicho kipo katika ziara ya kufanya
mikutano ya ndani.
Akizungumza ndani ya vikao hivyo, Lowassa pasipo kutaja jina la mtu yeyote alisema: “Mwacheni Mungu aitwe Mungu, kwa sababu wote hata walionisema mabaya baadhi yao wameshatangulia mbele ya haki.”
Alisema
kitendo cha wananchi kumpigia kura kwa wingi pamoja na kwamba alikuwa
akizungumziwa vibaya juu ya afya yake, ni wazi kuwa walikubali kubeba
lawama juu yake.
“Bila
ujasiri na umoja wa dhati, hawa jamaa wataendelea kutupiku… lakini
niwashukuru vile vile kwa kukubali kubeba lawama juu yangu, wapo
waliosema huyu ni mgonjwa atakufa, bado mlinipigia kura nyingi ila Mungu
ndiye hupanga yote,” alisema.
Pamoja
na hayo, Lowassa aliwataka wanachama wa Chadema kuendelea kuwa na
ujasiri na kudumisha umoja kwa kuendelea kujipanga kwa uchaguzi wa mwaka
2020.
Hii
ni mara ya kwanza kwa Lowassa kuzungumza juu ya watu ambao walihoji
kuhusu mwenendo wa afya yake wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Baadhi
ya wanasiasa, hususani wale waliokuwa wakimpinga, walijaribu kuionyesha
na hata kuiaminisha jamii kwamba mwanasiasa huyo ni mgonjwa na hafai
kuongoza nchi.
Wapo ambao walidiriki kusema kwamba Ikulu si hospitali na wala hakuna gari la kubebea wagonjwa.
Miongoni
mwa wapinzani wake ni baadhi ya wanasiasa wakubwa kutoka Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wakiwamo viongozi waliosikika katika majukwaa ya
kampeni mwaka jana wakiwashawishi wananchi kutomchagua Lowassa kwakuwa
hata akipata urais hatotawala muda mrefu atakufa.
Wapo
waliokwenda mbali na kusikika wakimwambia Lowassa Ikulu si wodi ya
wagonjwa, hivyo hafai kupatiwa nafasi ya urais kulingana na afya
aliyonayo.
Mikutano
ambayo Lowassa ameitumia kuzungumzia suala hilo, inafanyika nchi nzima
pamoja na kuwahusisha wajumbe wa ngazi mbalimbali za chama.
Uwepo wa Lowassa katika mikutano hiyo imesababisha watu wengi kukusanyika wakitaka kumuona.
Hata
Lowassa anapokuwa anaondoka katika eneo hilo kuelekea mahali kupumzika,
wananchi wamekuwa wakiunga msafara kwa kumfuata nyuma.
Mikutano hiyo inatajwa kuwa sehemu ya operesheni ya siku 40 inayofanyika nchi nzima iliyopewa jina la ‘Amsha Amsha’.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment