Siku zote hatutaacha kuzungumza juu ya mapenzi kwani ni ukweli
usiopingika kwamba mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha
yetu.
Tunafanya kazi usiku na mchana, tunahangaika huku na huko,
lakini mwisho tunafikiria jinsi gani tutaboresha na kufurahia maisha na
wapenzi wetu.
Mpenzi msomaji wangu, katika maisha ya kimapenzi
uaminifu ni kitu cha msingi. Bila uaminifu baina ya wawili waliotokea
kupendana, hakuna mapenzi na hata safari yao inaweza isifike mbali.
Kwa
sababu hiyo ndiyo maana wataalam wa mapenzi mara kwa mara wamekuwa
wakizungumzia suala hili kwa nguvu zote wakiamini ni mhimili muhimu
sana katika mapenzi.
Ifahamike kwamba uaminifu unaweza kujengwa. Kwa
mfano unaweza kuingia kwenye uhusiano na mtu kisha ukapata malalamiko
kutoka kwake kuwa, wewe si muaminifu. Katika mazingira haya ni suala la
kujiangalia tu na ili kuepusha mgogoro, tengeneza mazingira ya
kumfanya huyo mpenzi wako akuamini.
Unafanyaje? Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zinazoweza kukusaidia katika kujenga uaminifu katika ndoa yako:
1. Kuwa mkweli
Hakuna
kitu kibaya kama kuwa muongo kwa mwenzi wako. Unamfanya aamini kwamba
wewe si muaminifu kwake na ndiyo maana unadanganya bila sababu za
msingi. Kwa maana hiyo unachotakiwa kufanya ni kuwa mkweli kwake katika
kila jambo.
2. Timiza kwa wakati
Uaminifu pia unajengwa kwa
kutimiza mambo kadha wa kadha kwa mwenza wako hasa pale unapotoa ahadi.
Kwa mfano mmekubaliana mkutane maeneo flani saa 2:00 asubuhi, hakikisha
unakuwa pale kwa wakati. Huo ni mfano tu lakini kuna mambo mengi
ambayo unatakiwa kumtimiza mtu wako kwa wakati ili kujenga mazingira ya
wewe kuaminika.
3. Weka mipaka
Kama wewe ni mwanaume
hakikisha unajiwekea mipaka ya mazoea na wasichana wengine. Punguza
mazoea yasiyo ya lazima nao kwani hiyo inaweza kumjengea mpenzi wako
hisia kwamba unamsaliti.
Epuka kuwapa namba za simu watu ambao
wanaweza kukuletea usumbufu kwa mkeo. Epuka utani wa kijinga na watu wa
jinsia nyingine. Hii ni kwa mwanaume na mwanamke.
Ukijiwekea mipaka madhubuti utakuwa unamuweka mwenza wako katika mazingira ya kukuamini kwamba huwezi kushawishika kumsaliti.
4. Jiamini mwenyewe
Hili
ni la msingi sana. Kama unataka kujenga mazingira ya kuaminiwa anza
kujiamini mwenyewe. Kama utashindwa kujiamini hata mpenzi wako hawezi
kukuamini na matokeo uaminifu kati yenu hauwezi kuchukua nafasi.
5. Weka mambo sawa
Kwa
mfano mkeo anakutuhumu kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine. Kumbuka
hisia hizo hata kama hazina ukweli usipojitahidi kuziondoa kwake,
atajua ni kweli unamsaliti na ataamini hivyo katika kila siku ya maisha
yake.
Kwa mazingira hayo elewa uaminifu hauwezi kuwepo kati yenu
hivyo unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unamuweka sawa mpenzi wako na
kumfanya aondoe hisia hizo. Kwa kufanya hivyo utakuwa umejenga
mazingira ya uaminifu kati yenu.
Post a Comment