Kila kiumbe kina
utashi wa kupenda kwa vile upendo ndiyo tuliohimizwa sisi wanadamu,
lakini ukizidi unakuwa ugonjwa ambao huenda usipate dawa.
Naleta maada hii baada ya kupata swali kutoka kwa dada yangu mmoja
ambaye alitokea kumpenda kaka mmoja hadi kufikia kushindwa hata
kuzungumza pale anapomuona.Amejikuta akishindwa kujiamini
kujieleza kwa yule kaka na kuona hawezi kuzungumza chochote
kitakachoeleweka kwa vile amepoteza kujiamini kutokana na kumpenda
kupita kiasi.
Kupenda bila kujielewa ni sawa na wendawazimu, hata
unapokuwa ndani ya penzi hilo lililokutia wendawazimu, unapoteza
kujiamini kwa kuogopa kulipoteza penzi ulilolitafuta kwa muda mrefu.
Nimekuwa
nikielezea kujiamini kwa mwanadamu mbele ya mapenzi na kutojishusha
thamani hata kama umempenda mtu kupindukia. Kupenda ni haki yako ya
msingi lakini usiwe mtumwa wa mapenzi kwa kushindwa kujitambua wewe ni
nani na kwa nini upo pale.
Kupenda sawa, lakini ukizidisha inakuwa
sumu inayokutafuna taratibu kwa vile huna maamuzi yoyote ya moyo wako
kwa kuogopa kumuudhi umpendaye. Hii si kwa wanawake bali kwa watu wote.
Wapo
wanaofanyiwa vituko vya makusudi na wapenzi wao kwa vile tu wanatambua
wanapendwa na kukaa kimya kiasi cha kuwashangaza watu.
Kwa vile
hujiamini na mapenzi ndiyo yaliyochukua nafasi kubwa kwako na kuziba
mishipa ya ufahamu na kuamini hakuna mpenzi mzuri kama uliyenaye na
kuona kumpata kwako ni bahati, unakuwa huna maamuzi, kila utakaloambiwa
unaona sawa, liwe zuri au baya.
Hapa kidogo napenda mnisikilize kwa
makini, kila kiumbe kina haki ya kupenda, lakini lazima ujue
unayempenda kama kweli ana mapenzi ya dhati kwako. Kwa vile unampenda
unajitoa kwake kama kafara ya mapenzi na kuwa tayari kufanyiwa chochote
lakini usiachwe.
Tumeshuhudia wanawake kwa wanaume wakiteseka ndani
ya mapenzi yao kwa penzi la upande mmoja, unayalazimisha mapenzi kwa
vile tu unampenda na kuona hakuna kiumbe chochote mbele yako. Acha kuwa
kipofu wa mapenzi, siku zote mbegu ya upendo huota katika moyo wenye
rutuba ya upendo.
Usihadaike na rangi tamu ya chai sukari, matendo
mema ndiyo yanayojenga upendo ndani ya nyumba. Usiitupe ovyo mbegu yako
kwa vile tu umetokea kumpenda na kwamba kila ukimuona
unachanganyikiwa.
Je, unajua historia yake? Ana mapenzi ya kweli
kwako? Jiepushe kuutoa mwili wako ovyo kwa vile umependa tu bila kujua
mwenzako naye anakupenda.
Hata unayempenda ukimpata basi usikubali
kuwa mtumwa wa mapenzi, kwa penzi kukuongoza wewe na si wewe kuliongoza
penzi. Siku zote wewe ndiye uliongoze penzi na kutoa maamuzi pale
litakapokwenda kinyume.
Hii itakufanya uonekane mwenye msimamo na si mtu wa kuburuzwa.
Post a Comment