MFANYABIASHARA Robert Mwikwabe, maarufu kama Ndugu, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumpiga risasi ya kichwani na kusababishia kifo papo hapo mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya sekondari Sirari, Masaite Mrimi(17).
Kutokana na tukio hilo, Mwikwabe ambaye pia ni mmliki Hoteli katika mji mdogo wa Sirari wilayani Tarime mkoani Mara, alinusurika kuteketezwa yeye na familia yake Hali hiyo ilitokea baada ya wananchi kuamua kuchoma moto lori la mfanyabiashara hiyo na kwenda nyumbani kutaka kuchoma hoteli.
Mashuhuda walisema tukio hilo ni la juzi mchana, jirani na nyumba anayoishi mwanafunzi huyo, eneo la stendi mpya ya mabasi na malori ya Ngerengere.
Walisema mfanyabiashara huyo alifika akiwa na lori lake likiwa na mawe na alisimama na kutaka kuchukua pumba za mchele, zilizomwagwa na malori yanayosafirisha ng’ombe kwenda nchini Kenya.
Eneo hilo ni jirani na nyumbani kwao marehemu, ambako kulitokea mzozo kati ya Robert na wazazi wa mwanafunzi huyo. Kufuatia mzozo huo, mwanafunzi huyo aliyekuwa na panga mkononi, alimtishia kumkata Robert, ambaye alichomoa silaha yake aina ya bastola na kumpiga risasi kichwani na kumsababisha kifo.
Baada ya tukio hilo, familia ya marehemu na wananchi walianza kumfukuza Robert aliyeacha lori lake likiwa na mawe na kukimbilia lori lake lingine la jirani. Kisha alikimbilia Kituo cha Polisi Sirari, kuokoa maisha yake.
Umati mkubwa wa watu kutoka vijiji vya Ngerengere na Sirari, walikwenda nyumbani kwa mfanyabiashara huyo kwa lengo la kutaka kuchoma moto hoteli na nyumba.
Lakini, polisi na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga walifanya juhudi kubwa kuwazuia wananchi hasa vijana, kuacha kuteketeza mali za mfanyabiashara huyo yakiwemo magari, ambayo sasa yamehifadhiwa kituo cha polisi kwa ajili ya usalama.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Tarime-Rorya, Andrew Satta alithibitisha kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo na kwamba maiti imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Tarime.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment