DAR ES SALAAM: Hatari! Kuna
msemo kwamba, kila mtu anakula anapofanyia kazi, lakini ulaji mwingine
ni wa hatari sana! Mfano huu wa madai kwamba, baadhi (msisitizo baadhi)
ya watumishi kwenye baadhi ya hospitali na vyumba vya kuhifadhia maiti
(mochwari) jijini hapa wamekuwa wakiuza vitovu vya watoto wachanga na
maji yaliyooshea maiti, Uwazi limechimba.
Kwa mujibu wa chanzo, biashara hiyo hufanyika kwa siri kubwa kwani ni kinyume na utaratibu wa utendaji kazi wa hospitali husika.
TWENDE NA CHANZO
Kwa maelezo zaidi, chanzo kilisema: “Hii
biashara jamani imeshamiri sana. Ila sasa kuizima itakuwa ngumu kwa
sababu moja kuu, ni siri sana. Mnunuaji na muuzaji wanajuana.”
Maji ya maiti yakiuzwa.
BEI YAKE
“Kuhusu bei ni kama makubaliano. Lakini
iko hivi, maji yaliyooshea maiti ukiyataka kwenye chupa ya lita moja na
nusu ni shilingi laki moja (100,000), ila kama utalia sana, wanashusha
hadi shilingi elfu tisini (90,000).
“Kitovu kimoja cha kichanga ni shilingi elfu themanini (80,000), kama utalia sana mwisho ni elfu sabini (70,000).”
WATEJA WAKUBWA
“Katika kufuatilia, imegundulika kuwa,
wateja wakubwa sana ni waganga wa kienyeji. Hapa naomba nieleweke.
Namaanisha waganga wa kienyeji na si waganga wa tiba asilia au wa
mitishamba. Yaani wale wanaotibu zaidi kwa kutumia tunguli huku wakiwa
wamevaa shanga na mikia ya wanyama.
“Lakini mbali na wateja wakubwa kuwa
waganga, pia wapo watu ambao si waganga bali wamepewa masharti na
waganga. Kuna watu wakienda kwa waganga kuaguliwa, wanaambiwa ili tatizo
liishe, lazima apate maji ya maiti au kitovu cha mtoto mchanga.
KAZI YAKE KUBWA
“Kazi kubwa ya hivi vitu ni tiba, kuna
waganga wanatumia maji ya maiti kuagulia watu. Mfano wale wenye kesi
kubwa, magonjwa sugu, kuwazindua watu wanaoonekana kama mazezeta na pia
hutumia kukinga mashamba au biashara isikutwe na mikono ya wabaya.
“Lakini vitovu vya watoto pia vinatumika
kuzindikia nyumba, kuagulia utasa wa wanawake wanaosumbuka na kuzaa na
kuzuia wachawi kuingia ndani ya biashara au nyumba zile za kifahari.
“Pia vitovu hutumiwa na waganga katika kuwaumiza wanaume wanaotembea na wake za watu. Nasikia kuna dawa, hasa mkoani Tanga,
maeneo ya Handeni inajulikana kama usinga, mwanaume akitembea na mke wa
mtu anakufa mara moja. Sasa nasikia katika dawa hiyo, kitovu cha mtoto
kipo.”
SEHEMU HUSIKA
“Kama utataka maji yaliyooshea maiti
utauziwa na watu wanaofanya kazi mochwari, ingawa si kila mfanyakazi wa
mochwari anajihusisha na biashara hiyo. Ila wapo. Na kama utataka kitovu
cha mtoto, wauzaji wakuu ni baadhi ya wauguzi wasio waaminifu, ingawa
pia si wote,” kilisema chanzo.
MADAI YAFANYIWA KAZI
Ili kupata ukweli au uongo wa madai hayo, Uwazi
kwa kutumia waandishi wake wa kikosi cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’
wiki iliyopita lilifanya kazi ya kuzunguka kwenye hospitali ndogo na
kubwa za jijini Dar.
Baadhi ya hospitali (majina tunayo),
wauguzi wake walikuwa tayari kufanya biashara hiyo licha ya kwamba,
walionesha tahadhari kubwa wakati wa ‘kubageini’ bei.
OFM haikufikia hatua ya kununua kwa kuwaambia wahusika itarudi tena, lakini ukweli ukawa umejulikana kwamba, biashara hiyo ipo.
Katika hospitali moja, OFM ilikwenda
mpaka mochwari na kuzungumza kwa siri na mfanyakazi mmoja wa chumba
hicho ambaye alikubali kuuza maji yaliyooshea maiti kwa gharama ya
shilingi 90,000 baada ya kupunguza bei.
Mtu wa mochwari: “Sikia kijana. Bei ya
mwisho kabisa ambayo siwezi kupunguza zaidi ya hapo kwa maji ya maiti ni
shilingi elfu tisini. Kwa hiyo kama unayo lete pesa nikupe mzigo.”
OFM:
“Sawa, lakini anayehitaji ni kaka yangu, yeye ana kesi, mganga
kamwambia ampelekee maji ya maiti. Ngoja nimpigie ili ikibidi anitumie
pesa kwa mtandao wa simu.”
OFM alikwenda kusimama pembeni na
kuwasiliana na makao makuu ya kitengo hicho na kupewa maagizo kwamba,
aongee na mtu huyo kuwa biashara ifanyike nje ya mochwari ili OFM iweze
kupiga picha za kificho (kama machale yalimcheza), mhudumu huyo hakuwa
tayari.
OFM LASAKA MITAZAMO
Ili kupata mawazo mbalimbali na angalizo
pia, OFM iliwapigia simu baadhi ya watoa huduma ya utabibu jijini Dar
es Salaam, lakini aliyeweza kupatikana mara moja ni tabibu Maneno Tamba
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania.
Yeye alianza kwa kuambiwa kuhusu kuwepo kwa biashara hiyo ambapo alionesha kushtuka sana na kusema:
“Kwanza sijui kama kiungo cha binadamu
kinaweza kutumika kutibu. Lakini ni hatari sana. Mimi kwa upande wangu
kwanza sitibu kwa kutumia viungo vya binadamu wala kitu chochote
kinachotokana na mwili wa binadamu.
“Ila wateja wa hivyo vitu sijui watakuwa
akina nani? Maana bwana kuna waganga, kuna wanga, kuna wachawi na kuna
wajanja. Sasa sijui katika makundi hayo, kundi gani linaweza kununua
vitu hivyo lakini huenda lipo.”
OFM NA WAGANGA WAKUU WA MANISPAA
Pia, OFM liliwatafuta waganga wa
hospitali mbalimbali za jijini Dar. Awali, lilimtafuta Mganga Mkuu wa
Jiji, Judith Kahama lakini simu yake iliita bila kupokelewa. Na hata
alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (SMS) na kuambiwa kuhusu
madai hayo, hakujibu.
OFM lilifanikiwa kumpata Mganga Mkuu wa
Manispaa ya Ilala, Dk. Victorina Ludovick ambapo katika mazungumzo yake
ana kwa ana na OFM kuhusu kuwepo kwa madai hayo, alisema:
“Hilo suala sijawahi kulisikia. Ila kama
nyie mnaweza kufanya uchunguzi, andikeni barua kwa Afisa Habari wa Jiji
iende kwa Mkurugenzi wa Manispaa, akitoa ruhusa mfanye mnaweza
kutusaidia pia sisi.”
ANGALIZO
Muuguzi mmoja kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
alisema kuwa ni vizuri wanawake wanapokwenda kujifungua kuhakikisha
hakuna ujanjaujanja juu ya uhifadhi wa vitovu vya watoto wao.
“Ni kawaida kwa mzazi kupewa kitovu cha
kichanga chake kabla hajatoka hospitali ili akakifukie mwenyewe
anakotaka. Unajua mambo ya kitovu yana mila na desturi, nasi tunaheshimu
hilo. Sasa hao wenzetu wanaouza vitovu wanavipata wapi? Ina maana huwa
hawawapi wenyewe? Mimi nawaomba akina mama wawe makini,” alisema muuguzi
huyo.
OFM, juzi ilimpigia simu Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla
ili kusikia kutoka kwake, lakini simu yake haikuwa hewani. Hata
alipopigiwa waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu, naye simu yake haikuwa
hewani.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment