Azam FC imeamua kuwatimua makocha wake wa kigeni wakiongozwa na kocha mkuu Zeben Hernandez kutoka Hispania.
Uamuzi wa Azam umekuja baada ya mfululizo wa matokeo mabovu kwenye ligi kuu Tanzania bara msimu huu tangu ‘wahispaniola’ walipokabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo baada ya Stewart Hall kubwaga manyanga.
“Uongozi wa Azam FC umewatimua makocha wao leo mchana baada ya pande zote mbili kukubaliana kuvunja mkataba kutokana na matokeo mabaya kwenye ligi tangu walipowasili,” chanzo cha kuaminika toka ndani ya Azam FC kimeiambia shaffihdauda.co.tz.
Katika mechi 17 za VPL ambazo Hernandez alisimama kama kocha mkuu wa Azam FC, timu hiyo imeshinda mechi saba (7), imetoka sare mara sita (6) na kupoteza michezo minne (4).
Hadi sasa Azam ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa VPL ikiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 17. Azam inazidiwa pointi 14 na Simba ambao ndio vinara wa ligi huku wakiwa nyuma kwa pointi 10 dhidi ya Yanga huku wakizidiwa pointi moja na Kagera Sugar.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment