Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Raul Castro kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Cuba Mhe. Fidel Castro kilichotokea tarehe 25 Novemba, 2016. Katika Salamu hizo Rais Magufuli amesema;
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Fidel Castro. Kwa niaba ya Serikali, Wananchi wa Tanzania na kwa niaba yangu mwenyewe natoa pole nyingi kwako, familia, Serikali ya Cuba na wananchi wa Cuba kwa kumpoteza mtu muhimu.
Fidel Castro alikuwa kiongozi shupavu wa karne, atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na pia kwa misaada mikubwa aliyoitoa katika kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
Alikuwa rafiki wa Tanzania na Afrika nzima, historia ya Tanzania na Afrika haziwezi kukamilika bila kumtaja Fidel Castro, hakika kifo chake sio tu ni pigo kwa Cuba bali pia kwa Tanzania na Afrika.
Naungana nawe na wananchi wa Cuba katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, na pia nakuombea kwa Mwenyezi Mungu wewe, familia na wananchi wote wa Cuba muwe na nguvu, subira na ustahimilivu kutokana na kuondokewa na mpendwa wenu."
Pia Rais Magufuli amemuombea marehemu Fidel Castro apumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment