Akisoma hati ya mashtaka jana Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa kuwa mshtakiwa huyo alifanya hivyo na kujipatia dola za Marekani 540,390 kwa njia ya udanganyifu kati ya Februari 26 na Machi 3,2014.
Msigwa amedai kuwa Februari 20,2014 jijini Dar es Salaam, Ndama alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 yakiwa na thamani ya Dola za Marekani 8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Machi 6,2014 katika jiji la Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali (Certificate of Clearance) ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam, akijaribu kuonesha kilogramu 207 za dhahabu toka nchini Congo zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.
Wakili huyo wa Serikali ameendelea kudai kuwa Februari 20,2014 mshtakiwa huyo alighushi fomu ya forodha yenye namba za usajili R.28092 akionesha kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited imelipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa ambazo zina uzito wa kilogramu 207 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kutoka Congo kitu ambacho si kweli.
Pia, mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014 katika jiji la Dar es Salaam alijihusisha moja kwa moja na utakatishaji fedha kwa kufanya miammala ya dola za Marekani 540,390 kwa kuelekeza ziwekwe katika akaunti namba 9120000085152 iliyopo katika benki ya Stanbic yenye jina la Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited na kuzitoa taslimu wakati akijua fedha hizo zinatokana na zao la uhalifu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa hakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.
Upande wa mashtaka umedai upelelezi bado haujakamilika na mshtakiwa alipelekwa rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili ni miongoni mwa mashtaka yasiyo na dhamana.
Kesi imeahirishwa hadi Desemba 13,2016 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment