Siku tatu baada ya kudaiwa kumfanyia fujo jirani yake, Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo maarufu Mzee wa Upako, amejibu tuhuma hizo akisema anaishi kana kwamba hana jirani.“...Tunaishi kama majambazi tu, hujui jirani yako ni nani,” amesema.
Lusekelo amesema Yesu ambaye ni mwana wa Mungu alikubali kudhalilishwa na baadaye kufa bila hatia hivyo na yeye alikubali kula kiapo katika nafasi ya utumishi wake.
Amesema magazeti wa mitandao ya kijamii hayawezi kumshusha kwa kuwa hayakumpasha ila Mungu pekee.
Katika mahubiri yake yaliyohudhuriwa na waumini wengi kama ilivyo kwa Jumapili nyingine za karibuni kanisani kwake, Ubungo Kibangu, mchungaji huyo aliingia kwa mapokezi ya wimbo wa kuabudu uitwao ‘Angalia Bwana’ kabla ya waumini kuanza kumtunza kwa sadaka kama ilivyo kawaida ya ibada zake.
Katika mahubiri hayo alisema haiogopi jela, bali anaogopa kuvunja sheria za nchi na wala alipokamatwa na Polisi haikumtisha wala kumvunja moyo, kwani viongozi wa dini wamekula kiapo hadi kufa.
Aidha, alisema wapo waliosema kuwa Mzee wa Upako alikuwa anatukana, alidai kuwa matusi yake yote ni maandiko na anayetaka ufafanuzi wowote akipata nafasi amuulize yameandikwa katika vitabu gani li apate kuelewa.
Alisema mpumbavu sio tusi hayo ni maelezo na Yesu alitukanwa sana, na hata ushenzi si tusi lina maana pana ya kwamba huna hofu ya Mungu, mjinga ana dhambi ya mauti, inayomsubiri kwenda peponi.
Hata hivyo, aliwausia waumini wa kanisa hilo kuwa kamwe wasimtukane mtu kwa umbo ama rangi yake kwa kuwa hakupenda kuzaliwa hivyo na waishi hivyo kwa kutenda mema kwa kuwa ufalme wa Mungu watauona.
Alisema tangu kutokea kwa tukio amekuwa akipigiwa simu na watu ambao hakuwategemea huku waandishi wakimtaka kuzungumzia chochote wakiwamo waandishi wa habari ambao alisema walikuwamo ndani ya kanisa hilo jana.
Akifafanua kilichotokea siku hiyo, alieleza kuwa alitoka saa 11 alifajiri bila kufafanua alikuwa akitokea wapi, ndipo alipokutana na watu wawili akiwemo Mmasai na dada mmoja alipowauliza wanatokea wapi katika eneo hilo ambalo wakazi wengi wa huko hutoka na magari yao, ndipo ugomvi ulipoanzia.
“Hawa watu wa magazeti wanataka kuuza magazeti, barabara hiyo nimeijenga mimi hivyo nilikuwa na haki ya kuwauliza maana ni kibarabara... washenzi wakubwa wanaandika tu, halafu wanasema nimewatukana majirani kule hakuna jirani hajui wanaingia saa ngapi na wanatoka saa ngapi na hakuna hata habari za asubuhi. Kila mmoja anatumia gari lake,”alieleza Mzee wa Upako.
“Kwanza waliandika habari kwamba waumini hawatakuja kanisani badala yake wamejitokeza bila kukatishwa tamaa. Wakati mnajitokeza hapa mbele (kutoa sadaka), alipita mama mmoja amebeba mtoto, nilimwombea mwaka jana hapa kwamba atapata mtoto na leo amepata mtoto, sasa mbona magazeti yasiandike habari hizo?”
“Kwa nini wasiandike hayo mazuri ‘front page’ (ukurasa wa mbele)?, halafu mnaandika Mzee wa Upako matatani,matatani babu yako.”
“Najua na leo mmekuja mpo humu mnasubiri niseme, nasubiri mmalize kwanza nyinyi halafu na mimi ndiyo nitasema, baada ya mwezi mmoja najua mtakuwa mmemaliza,”alisema.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment