Nashukuru kupata fursa ya kuzungumza nanyi leo kuhusu hali ya uchumi
wa Taifa kwa kipindi cha Julai – Desemba, 2016 na matarajio hadi Juni
2017. Nitajitahidi kutumia lugha rahisi ili wananchi wa kawaida waweze
kuelewa mambo ya msingi kuhusu mwenendo wa uchumi wa nchi yetu.
Ustawi wa Uchumi Unapimwaje?
Ustawi
wa uchumi wa Taifa unapimwa kwa kuangalia viashiria mbalimbali. Kwa
kifupi, ustawi wa uchumi unapimwa kwa kuangalia kama shughuli mbalimbali
za kiuchumi zinaongezeka au zinapungua au kama zimedumaa.
Shughuli
muhimu zinazoangaliwa ni pamoja na uzalishaji wa chakula na mazao
mbalimbali ya kilimo, mifugo na uvuvi; uzalishaji wa bidhaa za viwandani
na migodini; ujenzi wa miundombinu; uwekezaji; mwenendo wa bei,
biashara na masoko; utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii ikiwa ni
pamoja na elimu, afya, maji, mawasiliano, usafiri na usafirishaji,
utalii na huduma za kifedha; na kiwango cha utekelezaji wa bajeti ya
Serikali.
Aidha, uchambuzi na tathmini ya hali ya uchumi wa Taifa
inafanyika kwa kulinganisha viashiria na malengo yaliyowekwa au kwa
kuangalia vigezo vinavyokubalika kimataifa au kwa kulinganisha na
mwenendo wa viashiria vya kiuchumi katika nchi nyingine. Vilevile, afya
ya uchumi inapimwa kwa kutumia vigezo vya jumla, vya kisekta na
kimaeneo.
- VIASHIRIA MBALIMBALI VYA MWENENDO WA UCHUMI WA TAIFA
- Ukuaji wa Pato la Taifa
Ukuaji wa uchumi (kasi ya kuongezeka au kupungua kwa uzalishaji
wa bidhaa na huduma katika nchi) ni mojawapo ya vitu vinavyotazamwa
katika kutathmini afya ya uchumi wa Taifa. Kiashiria kinachotumika
kupima ukuaji wa uchumi ni ukuaji wa Pato la Taifa yaani thamani ya
bidhaa na huduma zilizozalishwa katika nchi katika kipindi kinachorejewa
ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
Takwimu za ukuaji uchumi
zinaonesha kuwa uchumi wa Taifa umeendelea kukua na Tanzania imebaki
kuwa miongoni mwa nchi za bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara
ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa zaidi. Mwenendo wa ukuaji wa
uchumi kwa baadhi ya nchi jirani na kisekta umeoneshwa katika jedwali la
1 na la 2.
Jedwali1: Ukuaji wa Pato la Taifa Katika Baadhi ya Nchi za Kiafrika
NCHI | 2015 | 2016 |
Burundi | -4.0 | -0.5 |
Kenya | 5.6 | 6.0 |
Rwanda | 6.9 | 6.0 |
Tanzania | 7.0 | 7.2 |
Uganda | 4.8 | 4.9 |
Zambia | 3.0 | 3.0 |
Malawi | 2.9 | 2.7 |
Congo DRC | 6.9 | 3.9 |
Afrika Kusini mwa Sahara | 3.4 | 1.4 |
- Mfumuko wa bei
Kiashiria kingine cha jumla ni mfumuko wa bei ambao unapima
mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini.
Mfumuko wa bei ulipungua kutoka asilimia 6.5 Januari 2016 hadi asilimia
5.5 Juni 2016 na kupungua zaidi hadi asilimia 4.5 Septemba 2016 na
baadaye kupanda kidogo mwezi Novemba na kufikia asilimia 4.8. Maana yake
ni kuwa bei za bidhaa na huduma ziliongezeka kwa kasi ndogo zaidi
ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
Mwenendo huu wa kushuka
mfumuko ulichangiwa na kasi ndogo ya ongezeko la bei za chakula nchini,
kushuka kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia, utekelezaji
madhubuti wa sera za bajeti na fedha, na utulivu wa thamani ya Shilingi.
Kupanda kwa mfumuko wa Bei mwezi Novemba kulitokana na kupungua kwa
upatikanaji wa bidhaa za chakula (mbogamboga, unga wa mahindi na ngano)
pamoja na mkaa.
Mfumuko wa bei katika nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki: Wastani wa mfumuko wa bei uliendelea kubakia katika wigo wa
tarakimu moja.
Hata hivyo, mwezi Novemba 2016, karibu nchi zote zilikuwa
na ongezeko la mfumuko wa bei kutokana na kuyumba kwa ugavi wa chakula
katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupanda kwa bei za mafuta
katika soko la dunia.
Nchini Uganda, mfumuko wa bei uliongezeka kufikia
asilimia 4.6 Novemba 2016 ikilinganishwa na asilimia 4.1 Oktoba 2016.
Aidha, mfumuko wa bei nchini Kenya ulipanda na kuwa asilimia 6.68
ikilinganishwa na asilimia 6.47 katika kipindi hicho.
Matarajio
kwa mwaka 2017 ni kubaki na mfumuko wa bei katika kiwango cha tarakimu
moja. Hata hivyo upungufu wa mavuno ya mazao ya chakula uliojitokeza kwa
baadhi ya nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika unaweza kusababisha
shinikizo la mfumuko wa bei katika siku za usoni.
- Thamani ya shilingi
Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani
imeendelea kuimarika. Shilingi imekuwa ikibadilishwa kwa kati shilingi
2,167 hadi 2,199 kwa dola moja ya Marekani.
Hali hii ilitokana na
kuwa sera thabiti za uchumi pamoja na mwenendo mzuri wa urari wa mapato
ya fedha za kigeni hususan kutokana na mauzo ya bidhaa za viwandani,
utalii na huduma mbalimbali.
- Mwenendo wa Sekta ya Kibenki
Tathmini ya hali ya mabenki yetu inaonesha kuwa mabenki yetu ni imara na salama, yakiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha:
Kiwango
cha mitaji kikilinganishwa na mali iliyowekezwa (total capital to total
risk weighted assets and off-balance sheet exposures) kilikuwa asilimia
18.68 kikilinganishwa na kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria cha
asilimia 12.0.
Hali ya ukwasi hupimwa kwa kuangalia uwiano kati ya
mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu na amana zinazoweza
kuhitajika katika muda mfupi (liquid assets to demand liabilities).
Uwiano huu ulikuwa asilimia 37.46 ukilinganishwa na uwiano wa chini
unaohitajika kisheria wa asilimia 20.
Amana za wateja katika
mabenki zilipungua kidogo kutoka shilingi trilioni 20.73 mwezi Desemba
2015 kufikia shilingi trilioni 20.57 mwezi Septemba 2016. Miongoni mwa
sababu zilizochangia kupungua kwa amana kwenye mabenki ni pamoja na
uamuzi wa Serikali kuhamisha sehemu ya fedha za taasisi na mashirika ya
umma kutoka mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo
amana za serikali kwenye mabenki ya biashara ni asilimia 3 tu ya amana
zote za mabenki.
Upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi
wasiofikiwa na mabenki umeendelea kuongezeka kutokana na ubunifu wa
mipango ya utoaji wa huduma za malipo ya rejareja kupitia simu za
mikononi, pamoja na huduma za uwakala wa mabenki (agent banking
services).
Benki zilizopata msukosuko: Katika kipindi cha Julai –
Septemba 2016, CRDB na TIB Development Bank zilipata hasara. Hasara
ilisababishwa na tengo kwa ajili ya mikopo chechefu (provision for loan
losses). Aidha, Twiga Bancorp imewekwa chini ya uangalizi wa BOT, jambo
ambalo si geni. Crane Bank Ltd ya Uganda imewekwa chini ya usimamizi wa
Benki Kuu ya nchi hiyo Oktoba 2016 kama ilivyokuwa Imperial Bank Kenya,
Oktoba 2015.
Licha ya hali hiyo, benki nyingi zikiwamo CRDB na TIB
Development Bank, zimebaki kuwa na mitaji na ukwasi wa kutosha kwa
mujibu wa Sheria. Aidha ni vema kukumbuka kwamba jumla ya benki na
taasisi za fedha nchini kote ni 66 na zina matawi 783. Hivyo, kwa benki
tatu (3) tu kupata msukosuko katika robo moja ya mwaka si sababu ya
kuzua taharuki!
Mwenendo wa mabenki katika nchi nyingine Afrika:
Kupungua kwa mikopo kwa sekta binafsi katika miezi ya hivi karibuni siyo
kwa Tanzania pekee. kwa mfano kiwango cha ukuaji cha ukuaji wa mikopo
kwenda sekta binafsi katika nchi jirani ya Kenya kilipungua kutoka
asilimia 19.7 kati ya Julai na Oktoba 2015 hadi kufikia asilimia 4.1
katika kipindi kama hicho katika mwaka huu 2016.
Aidha huko Uganda
mikopo kwa sekta binafsi ilipungua kutoka asilimia 25.2 mwezi September
2015 hadi asilimia -1 mwezi September 2016.
Pia mwenendo usioridhisha
ulijitokeza katika mikopo chechefu katika nchi hizo jirani na
kusababisha baadhi ya mabenki hususan Crane Bank ya Uganda na Imperial
Bank ya Kenya, kuwekwa chini ya uangalizi. Hali ni mbaya zaidi kwa nchi
kama Nigeria na Ghana zinazouza mafuta.
Ujazi wa fedha kwa tafsiri
pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 4.5 katika kipindi cha mwaka
ulioishia Oktoba 2016 (au ongezeko la shilingi bilioni 547.3)
ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 16.6 (au ongezeko la shilingi
bilioni 3,084.6) kwa mwaka ulioishia Oktoba 2015. Ukuaji mdogo
unatokana na usimamizi madhubuti wa matumizi sambamba na kupungua kwa
fedha za misaada na mikopo kutoka nje.
Kwa upande wa mikopo kwa
shughuli za biashara na za binafsi ilikuwa asilimia 39 ya mikopo yote.
Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa shilingi bilioni 1,550.5 hadi
shilingi bilioni 16,654.4 katika mwaka unaoishia Oktoba 2016, sawa na
ukuaji wa asilimia 10.3 ikilinganishwa ongezeko la shilingi bilioni
2,977.6 au ukuaji wa asilimia 24.6 katika kipindi kinachoishia Oktoba
2015.
Katika kipindi cha Julai – Oktoba 2016 mwenendo wa riba za amana
na za mikopo umekuwa wa kupanda na kushuka. Wastani wa riba za amana
ulikuwa asilimia 9.49 ukilinganisha na wastani wa asilimia 9.08 katika
kipindi kama hicho mwaka 2015. Aidha, wastani wa jumla wa riba za mikopo
ulikuwa asilimia 15.85 ikilinganishwa na asilimia 16.11 katika kipindi
kama hicho mwaka 2015.
Mwenendo wa riba za mikopo unategemea mambo
mbalimbali kama vile, gharama ya fedha (cost of funds), gharama za
uendeshaji wa benki husika (bank’s operational cost), kiwango cha faida
(profit margin), mfumuko wa bei na vihatarishi vinavyotokana na sifa za
mkopaji (risk premium). Viwango vya riba katika masoko ya fedha
vimeendelea kutegemea nguvu ya soko na hali ya ukwasi unaotokana na sera
za fedha na kibajeti.
- Sekta ya Nje na Akiba ya Fedha za Kigeni
Hadi kufikia Novemba 2016, nakisi ya urari wa biashara ya
bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje (current account deficit)
ilipungua kwa asilimia 52.5 na kufikia nakisi ya dola za Kimarekani
milioni 1,904.2, kutoka nakisi ya dola za Kimarekani milioni 4,008.3
katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
Kupungua huko kulitokana na
ongezeko la thamani ya madini hususan dhahabu, bidhaa asilia, mapato
yatokanayo na utalii, pamoja na kupungua kwa thamani ya bidhaa
zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususan bidhaa za mitaji, na bidhaa za
matumizi ya kawaida. Katika kipindi hicho thamani ya bidhaa na huduma
zilizouzwa nje ya nchi ziliongezeka kwa asilimia 6.4 na kufikia dola za
Kimarekani milioni 8,502.8 wakati thamani ya bidhaa na huduma toka nje
zilipungua kwa asilimia 15.4 na kufikia dola za Kimarekani milioni
9,846.0.
Hadi mwezi November 2016, akiba ya fedha za kigeni
ilifikia dola za Kimarekani milioni 4,254.1 ambazo zinatosheleza kuagiza
bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4. Wakati huo
huo, rasilimali za fedha za kigeni za mabenki (gross foreign assets)
zilikuwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 777.0 Hivyo, akiba ya
fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha.
Jedwali 2: Viashiria vya Ustawi wa Uchumi
ENEO | KIASHIRIA | JUL – SEPT 2015 | OCT – DES 2015 | JUL – SEPT 2016 | OCT – DES 2016 | 2016 | |
Ukuaji wa Uchumi | Ukuaji wa Pato la Taifa | 6.3% | 9.1% | 6.2% | 8.0% | 7.2% | |
Sekta zenye mchango mkubwa ktk Pato la Taifa | Kilimo (35.8%); Ujenzi (12.4%); Biashara (9.7%) | Kilimo (28.3%); Ujenzi (11.0%); Biashara (10.7%); Viwanda (6.3%) | Kilimo (24.7%); Ujenzi (14.6%); Biashara (10.3%); Viwanda (7.3%); Madini (5.2%) | ||||
Sekta zilizokua haraka | Ujenzi (17.6%); Usafirishaji & Uhifadhi (10.6%); Mawasiliano (9.1%); Huduma za kifedha (8.4%); Madini (8.0%) | Madini (15.750; Ujenzi (13.8%); Huduma za kifedha (12.6%); Mawasiliano (10.2%); Viwanda (9.5%) | Madini (19.9%); Mawasiliano (14.3%); Usafirishaji (12.2%); Nishati (11.8%); Huduma za kifedha (8.7%); | ||||
Sekta zilizokua polepole | Kilimo (2.7%); | Kilimo (0.3%) | |||||
Bei, Biashara na Masoko | Mfumuko wa bei | 5.3% | 6.6% | Jul (5.1%)Ago (4.9%) Sep (4.5% | Okt (4.5%),Nov (4.8%) | 5.5% | |
Nakisi kwenye Biashara ya Nje (US$ Milioni) | |||||||
Mwenendo wa Sekta ya Fedha | Akiba ya fedha za Kigeni (US$ milioni) | 3,999.3 | 4,093.7 | 4,096.0 | 4,254.1 | 4,654.2 | |
Kiwango cha Kubadilisha Fedha (Tshs; 1US$) | 2,150.0 | 2,148.5 | 2,175.32 | 2,170.97 | |||
Uwiano wa mikopo na Amana za wateja katika mabenki | 77.16 | 78.88% | 71.16% | ||||
uwiano wa jumla ya mitaji na mali iliyowekezwa (Total capital/Total risk weighted assets) | Sept (18.68%) | 19.4% (Des) | Sept (18.68%) | 12% | |||
uwiano wa raslimali inayoweza kubadilishwa kirahisi kuwa fedha taslim na amana zinazohitajika katika muda mfupi (Liquid assets/Demand liabilities) | Sept (37.46%) | Des (37.18%) | Sept (37.46%) | 20% | |||
Riba za Mikopo ya mwaka mmoja | Sept (14.4%) | Okkt (14.27%) | Sept (13.4%) | Okt (13.23%) | |||
Riba za amana za mwaka mmoja | Sept (10.6%) | Okt (10.95%) | Sept (11.5%) | Okt (11.46%) | |||
Amana za wateja | Sept (Tshs19.892 trillion) | Okt (Tshs19.995 trillion) | Sept (Tshs20.73 trillion) | Okt (Tshs20.98 trillion) | |||
Mikopo chechefu | Sept (6.62) | Des (6.64) | Sept (8.26) |
- MWENENDO WA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI 2016/17
- Mwenendo wa Mapato
Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali ilipanga kukusanya na
kutumia shilingi bilioni 29.539.6. Katika kipindi cha miezi mitano ya
kwanza ya mwaka 2016/17, makusanyo ya ndani ikijumuisha mapato ya
Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 7,018.7 sawa na asilimia 96.4 ya
makadirio ya shilingi bilioni 7,281.2 katika kipindi hicho
Mapato ya kodi
Mapato
ya kodi yalifikia shilingi bilioni 5,674.7 ikiwa ni asilimia 96.6 ya
lengo la kukusanya shilingi bilioni 5,873.3 kwa kipindi hicho. Aina za
kodi zilizofanya vizuri ni pamoja na kodi ya Ongezeko la thamani ndani,
ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa nje.
Hii ilitokana na usimamizi
thabiti wa makusanyo kwenye malimbikizo ya kodi, ukaguzi na uchunguzi wa
marejesho ya kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT returns) na kodi ya
mapato uliofanyika katika kipindi hicho, kupanua wigo wa kodi kwa
kusajili walipa kodi wapya, pamoja na utekelezaji wa mikakati ya
kuongeza makusanyo ya kodi.
Mapato yasiyotokana na kodi
Mapato
yasiyotokana na kodi yalifikia shilingi bilioni 1,133.4 sawa na
asilimia 0.2 zaidi ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 1,130.6.
Sababu za kuvuka lengo ni kutokana na kuongezeka kwa mapato yasiyo ya
kodi yanayokusanywa na TRA ikijumuisha kodi ya majengo pamoja na kufanya
vizuri kwa Wizara na Mikoa zinazokusanya maduhuli.
- Aina za kodi ambazo hazikufikia lengo
Aidha, aina za kodi ambazo hazikufikia lengo ni pamoja na ushuru
wa bidhaa ndani, kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) nje, kodi ya mapato
na kodi nyingine hasa ushuru wa stamp (stamp duty) na Departure fee.
Sababu zilizopelekea kutokufikiwa kwa malengo la ukusanyaji wa mapato ya kodi:
- Kushuka kwa mauzo ya bidhaa mbalimbali kama vile saruji, bia, vinywaji baridi na bidhaa nyinginezo za jumla na rejareja kumesababisha makampuni mengi kutopata faida ilivyotarajiwa na hivyo kupunguza wigo wa ukusanyaji wa kodi;
- Mabenki makubwa yalifanya marekebisho ya makisio yao ya kulipa kodi kutokana na kushuka kwa mapato ya riba;
- Kupungua kwa uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia ambako kuliathiri kodi ya zuio na kodi ya mapato;
- Ajira kutoongeza kama ilivyotarajiwa baada ya kusitisha ajira mya ili kupisha zoezi la kubaini watumishi hewa serikalini;
- Baadhi ya kampuni kupunguza bei katika baadhi ya bidhaa kama vile bia ili kuongeza mauzo yao;
- Kuongezeka kwa malimbikizo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye sekta ya uzalishaji wa umeme hususan IPTL na Symbion Power Ltd;
- Matumizi hafifu ya mashine za kielektroniki (EFD);
- Kupunguza kwa ulaji wa bidhaa zinazotozwa kodi na ushuru wa bidhaa husuan bia, vinywaji vikali na vinywaji baridi;
- Matatizo ya kifedha yaliyokumba kampuni za usafirishaji wa anga pamoja na kupungua kwa idadi ya wasafiri hususan wa sekta ya umma (departure charges); na
- Kushuka kwa uingizaji wa bidhaa kutoka nje.
Hatua za kuimarisha ukusanyaji wa kodi ili kufikia malengo katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2016/17:
- Kupanua wigo wa kodi kwa kuendelea kusajili na kuhakiki taarifa za walipakodi kwenye mifumo ya kikodi ya TRA;
- Kuendelea kushirikiana na Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi kwa kubadilishana taarifa;
- Kuendelea kusimamia na kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFDs);
- Kudhibiti udanganyifu katika ukadiriaji wa kodi kwa kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa walipakodi;
- Kuimarisha ukaguzi wa kodi (tax audit);
- Kudhibiti na kusimamia bidhaa zinazopitia hapa nchini kwenda nchi jirani (transit) kwa kutumia mfumo wa kufuatilia mizigo (electronic cargo trackin system);
- Kuboresha ukaguzi wa mizigo bandarini; na
- Kudhibiti biashara ya magendo hususan katika Bahari ya Hindi, mipaka na njia zisizo rasmi kati ya nchi yetu na nchi jirani.
- Misaada na Mikopo Yenye Masharti Nafuu
Katika mwaka 2016/17 Washirika wa Maendeleo waliahidi kuchangia
bajeti ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 3,600.8, ambapo kati
ya hizo, misaada ya Kibajeti ni shilingi bilioni 483.0, Mifuko ya
Kisekta ni shilingi bilioni 372.1 na miradi ya Maendeleo ni shilingi
bilioni 2,745.7. Jumla ya misaada na mikopo nafuu iliyotolewa kwa
kipindi cha Julai hadi Novemba 2016 ni shilingi bilioni 603.9 sawa na
asilimia 21.5 ya lengo la shilingi bilioni 2,806.3 katika kipindi hicho.
Misaada:
Kati ya Julai hadi Novemba 30, 2016, misaada ya kiasi cha shilingi
bilioni 287.5 ilitolewa, sawa na asilimia 28.4 ya lengo la shilingi
bilioni 1,012.6 kwa kipindi hicho. Kati ya kiasi hicho, misaada ya
kibajeti (General Budget Support) ni shilingi billioni 36.1 ambazo zote
zimetolewa na EU tu; na kiasi kilichopokelewa kwa ajili ya mifuko ya
kisekta (Basket Funds) ni shilingi bilioni 58.4, sawa na asilimia 61 ya
lengo ya shilingi bilioni 95.5 kwa kipindi hiki cha marejeo. Aidha,
misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kipindi hicho ilifikia
shilingi bilioni 193.1, ambayo ni asilimia 21 ya lengo la shilingi
bilioni 917.1 kilichotarajiwa kupokewa kwa kipindi hicho.
Mikopo
nafuu iliyopokelewa kutoka kwa washirika wa maendeleo kwa ajili ya
miradi ya maendeleo kati ya Julai hadi Novemba, 2016 ni shilingi bilioni
316.4. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 17.6 ya lengo la shilingi bilioni
1,793.7. Aidha, katika kipindi hicho, hakuna mikopo nafuu iliyopokelewa
kwa ajili ya mifuko ya kisekta na programu (GBS).
Sababu za
kutofikiwa malengo ya upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu ni pamoja
na masharti magumu yaliyowekwa na wahisani/wakopeshaji. Hata hivyo,
Serikali inatarajia kukamilisha majadiliano na AfDB kati ya mwezi
Desemba 2016 hadi Machi, 2017.
Aidha, majadiliano na Benki ya Dunia na
Umoja wa Ulaya, bado yanaendelea. Kuhusu fedha za miradi, jitihada
zinafanyika katika sekta husika kukamilisha taarifa za miradi
zinazohitajika na wafadhili.
Mikopo ya ndani
Katika
kipindi cha Julai – Oktoba 2016, shilingi bilioni 1,367.2 zilikopwa
katika soko la ndani. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 1,305.7
zilikopwa kwa ajili ya kulipia dhamana na hatifungani za Serikali
zilizoiva na shilingi bilioni 61.5 zilikuwa ni malipo ya marejesho
(repayment). Kiasi kilichokopwa katika kipindi hiki ni sawa na asilimia
58 ya kiasi kilichopaswa kukopwa cha shilingi bilioni 2,232.5.
Mikopo ya Kibiashara
Katika
mwaka 2016/17, Serikali ilipanga kukopa fedha kutoka kwenye vyanzo vya
kibiashara kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 936
sawa na shilingi bilioni 2,100.9 ili kugharimia miradi mbalimbali
ya maendeleo. Hata hivyo, hadi kufkia Novemba, 2016 Serikali haikukopa
kutoka katika chanzo hiki kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa
kutokuwa nzuri hasa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2016/17.
Hali
hii ilisababishwa na mdodoro wa kiuchumi katika bara la Ulaya na hivyo
kuongezeka kwa gharama za mikopo mipya na kuathiri upatikanaji wake.
Mfano, riba ilipanda kutoka wastani wa asilimia 6 hadi asilimia 9.
Kutokana na sababu hiyo, Serikali iliahirisha kuendelea na mchakato wa
kukopa kutoka kwenye masoko hayo na badala yake ikajielekeza kukopa
kutoka nchi nyingine (China, India, Korea Kusini, Japan).
Aidha, gharama
za ukopaji katika masoko ya ulaya imeanza kuimarika na hivyo Serikali
imeanza majadiliano na Benki ya Credit Suissuie ya Uingereza ili
tuweze kukopa dola za kimarekani milioni 300. Vilevile
majadiliano na taasisi nyingine za fedha kama Kuwait Fund, Abu
Dhabi Fund na OPEC yameendelea kwa ajili ya kugharamia miradi
mbalimbali.
Mwenendo wa Matumizi
Sera za Bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2016/17, zililenga kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za
umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na miongozo
mbalimbali. Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba
mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha
kwenye miradi ya maendeleo.
Fedha zilizotolewa Julai – Novemba, 2016
Katika
kipindi cha Julai – Novemba, 2016 jumla ya Shilingi bilioni 9,481.260
zilitolewa na Hazina kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Sekretarieti za
Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
- Shilingi bilioni 7,295.455 zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya Kawaida (ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri Shilingi 61.047)
- Mishahara ya Watumishi wa Serikali Shilingi 2,834.695,
- Deni la Taifa Shilingi bilioni 3,552.249
- Matumizi Mengineyo Shilingi bilioni 928.511
- Shilingi bilioni 2,185.805 kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo (ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri shilingi bilioni 91.571)
- Fedha za ndani Shilingi bilioni 1,749.047
- Fedha za nje Shilingi bilioni 436.758
- Maeneo ya Msingi ambayo fedha zimeelekezwa
Matumizi ya kawaida yaliyopewa kipaumbele zaidi katika utoaji wa fedha kwa kipindi cha Julai – Novemba 2016 ni pamoja na:
- Uboreshaji wa huduma za afya katika ngazi zote ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba Shilingi bilioni 69.346;
- Mitihani ya darasa la nne na saba Shilingi bilioni 33.745;
- Mitihani ya kidato cha pili na nne Shilingi bilioni 31.051;
- Posho ya chakula kwa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama;
- Chakula cha wafungwa Shilingi bilioni 7.5;
- Mishahara ya watumishi wa Serikali;
- Elimu msingi bila malipo Shilingi bilioni 93.885 (kwa kutenga shilingi bilioni 18.777 kila mwezi);
- Malipo ya posho na stahili mbalimbali kwa maafisa katika balozi zetu nje shilingi bilioni 23.127;
- Ruzuku ya pembejeo shilingi bilioni 10.00;
- Ununuzi wa chakula cha Hifadhi ya Taifa shilingi biliioni 9.00.
- Deni la kuchapisha Vitabu vya Hati za Kusafiria Shilingi 2.569;
- Uendeshaji wa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge, Mkutano wa Bunge, Posho ya Jimbo kwa Wabunge pamoja na shughuli za Mfuko wa Bunge Shilingi bilioni 31,137;
- Michango ya Taasisi na Jumuiya za Kimataifa Shilingi billion 8.833;
- Ruzuku ya Vyama vya Siasa Shilingi bilioni 7.168;
Aidha, sehemu iliyosalia ya fedha za Matumizi ya Kawaida
ilielekezwa kwenye shughuli za kila siku za uendeshaji katika Mafungu
mbalimbali.
Matumizi ya Maendeleo yaliyopewa kipaumbele kwa kipindi cha miezi mitano ni pamoja na:
- Ununuzi wa ndege mbili za Serikali Shilingi bilioni 103.386 na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege 4 shilingi bilioni 91.533;
- Usambazaji wa umeme vijijini Shilingi bilioni 266.493;
- Ujenzi na ukarabati wa barabara Shilingi bilioni 335.931;
- Usambazaji wa maji vijijini na mijini Shilingi bilioni 65.2445;
- Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu Shilingi bilioni 210.758;
- Mfuko wa Reli Shilingi bilioni 42.404;
- Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma na Mwanza Shilingi bilioni 12.353;
- Ujenzi wa majengo ya utawala katika Wilaya mpya na Mamlaka za Serikali za Mitaa Shilingi bilioni 11.00;
- Ujenzi na ukarabati wa ofisi za Halmashauri Shilingi bilioni 30.10;
- Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo Tanzania bara Shilingi bilioni 9.0; na
- Uboreshaji wa miundombinu ya shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum Shilingi bilioni 2.5.
- Ulipaji wa Madai mbalimbali
Katika kipindi cha Julai – Novemba, 2016 madai yaliyohakikiwa ya
jumla ya Shilingi bilioni 318.556 yalilipwa, ambapo shilingi bilioni
183.714 ni kwa ajili ya Wakandarasi na Wahandisi Washauri wa miradi ya
barabara; Shilingi bilioni 42.951 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji;
Shilingi bilioni 30.00 kwa ajili ya mikataba ya ulinzi na usalama;
Shilingi bilioni 25.00 kwa ajili ya miradi ya umeme; Shilingi bilioni
15.439 kwa ajili ya wazabuni mbalimbali; shilingi bilioni 10.00 kwa
ajili ya madai ya watumishi; Shilingi bilioni 7.00 kwa ajili ya matibabu
nje ya nchi (Hospitali ya Apollo, India); Shilingi bilioni 3.150 kwa
ajili ya Mtaalam Mwelekezi wa mipango miji ya jiji la Arusha na Mwanza;
na shilingi bilioni 1.302 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali ya
Serikali.
Deni la Taifa
Deni la Taifa limeendelea kuongezeka
na kufikia dola za Kimarekani milioni 21,087.9 mwishoni mwa mwezi
October 2016, kutoka dola za Kimarekani milioni 19,861.1 mwezi Desemba
2015.
Deni la nje liliongezeka kwa asilimia 3.4 na kufikia dola za
Kimarekani milioni 16,407.6 mwezi October 2016 (sawa na asilimia 77.8
ya deni la taifa), kutoka dola za Kimarekani milioni 15,863.9 mwezi
Desemba 2015. Hii ilitokana na kuongezeka kwa mikopo mipya pamoja na
malimbikizo ya malipo ya madeni. Katika deni hilo la nje, asilimia 83.0
ni deni la Serikali na taasisi za umma.
Deni la ndani liliongezeka
kufikia shilingi bilioni 10,089.3 mwishoni mwa mwezi Octoba 2016 kutoka
shilingi bilioni 8,597.0 mwezi Desemba 2015. Ongezeko hilo lilitokana
na Serikali kukopa kupitia dhamana na hati fungani kwa ajili ya
kugharamia bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, ikichangiwa pia na
kupungua kwa misaada na mikopo kutoka nje.
Deni la Taifa ni
himilivu: Pamoja na kuongezeka huko, deni la Taifa bado ni himilivu.
Uchambuzi wa Uhimilivu wa Deni uliofanyika mwezi Novemba 2016 unaonesha
kuwa viashiria vya deni la nje na deni lote la umma viataendelea kuwa
chini ya ukomo wa uhimilivu katika kipindi cha muda mfupi, muda wa kati
na muda mrefu. Uchambuzi unaonesha kuwa viashiria vyote vitaendelea kuwa
chini ya ukomo wa kimataifa hivyo deni la Taifa ni himilivu.
Changamoto
Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kadhaa zilijitokeza zikiwemo:-
- Baadhi ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kutokuwa na mwamko wa matumizi ya mashine za kielektroniki;
- Ukusanyaji usioridhisha wa maduhuli ya Serikali;
- Kushindwa au kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje;
- Maombi ya misamaha ya kodi; na
- Mahitaji makubwa (yasiyowiana na hali halisi ya upatikanaji wa mapato) ya kuboresha miundombinu hususan ya maji, reli, bandari, viwanja vya ndege na barabara;
- MAENEO YANAYOLALAMIKIWA NA BAADHI YA MAGAZETI NA KWENYE MITANDAO
4.1 Kupungua kwa Ukwasi Kufuatia Uamuzi wa Serikali Kuzitaka Taasisi za Umma Kufungua Akaunti za Mapato Benki Kuu
Uamuzi
wa Serikali kuzitaka taasisi za umma kufungua akaunti ya mapato Benki
Kuu utaendelea kubaki kama ulivyo. Kwa kifupi, fedha hizi za umma
zilikuwa zinatumika vibaya na Bodi za mashirika lakini pia zilitumika
kuikopesha Serikali fedha zake yenyewe kwa riba kubwa kupitia biashara
ya dhamana na hati fungani za Serikali. Kasoro hiyo iliondoa motisha kwa
mabenki ya biashara kupeleka huduma za kifedha vijijini na hata
kukopesha sekta binafsi (crowding out credit to the private sector).
Aidha,
ni vyema jamii ya Watanzania ikafahamu kwamba akaunti ambazo fedha za
mashirika zimehamishiwa Benki Kuu ni akaunti za kukusanya mapato tu.
Akaunti za matumizi bado ziko katika benki za biashara ili kuyawezesha
mashirika kufanya malipo kupitia akaunti hizo. Hivyo, bado benki za
biashara ni kiungo muhimu kati ya mashirika ya umma na watoa huduma kwa
mashirika hayo.
Hatua iliyochukuliwa na Serikali inalenga kuzisukumu
benki za biashara kuchukua hatua za ziada kupanua huduma za kifedha hadi
vijijini badala ya kujikita mijini zaidi kuhudumia makampuni makubwa
(corporate sector) na kufanya biashara katika soko la dhamana na hati
fungani za Serikali.
4.2 Mkikimkiki wa Ukusanyaji Kodi umekimbiza Wapangaji wa Majengo Marefu na Kusababisha Biashara Nyingi Kufungwa
Taarifa
kutoka Mfuko wa Pensheni wa PPF zinaonesha kuwa kati ya majengo 15
inayomiliki sehemu mbalimbali nchini, mtiririko wa wastani wa wapangaji
uko kama ifuatavyo:
- Majengo saba (7) yana wapangaji kwa asilimia 100 hadi kufikia Desemba 14, 2016;
- Jengo moja (DICC – PPF Tower) kwa sasa halipangishwi bali linaendeshwa na PPF wenyewe kama ukumbi wa mikutano;
- Jengo moja (PPF Plaza – Arusha) ni jipya na idadi ya wapangaji imeshaanza kuongezeka kutoka asilimia 34 mwezi Machi 2016 lilipofunguliwa hadi asilimia 39.1 Desemba 2016;
- PPF Kijitonyama ina nyumba nne (4) na kati ya hizo, mbili tu zenye wapangaji. Hatua za kutafuta wapangaji zinaendelea;
- PPF Kaloleni Arusha ina nyumba 20 na mwenendo wa wapangaji ulikuwa ukipanda na kushuka na katika kipindi kilichoishia Desemba 2016 umeongezeka kufikia asilimia 75 kutoka asilimia 65 mwezi Juni 2016;
- Majengo manne yaliyobaki (PPF Tower and Parking Arcade, PPF Plaza Mwanza, PPF House na PPF Olerien Estate) idadi ya wapangaji ilipungua na kufikia wastani wa asilimia 78.5 kwa yote katika kipindi kilichoishia Desemba 2016 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 84.8 Juni 2016.
Aidha, taarifa kutoka PSPF zinaonesha kuwa katika majengo manne
(4) inayomiliki imeweza kukodisha jumla ya futi za mraba 58,119.33
katika kipindi kilichoishia Juni 2016 ikilinganishwa na futi za mraba
57,883.5 zilizokodishwa hadi Juni 2015, sawa na ongezeko la asilimia
0.4.
Katika kipindi hicho kilichoishia Juni 2016, eneo lililokodishwa
katika majengo ya Jubilee na PSPF Plaza lilipungua kwa asilimia 4.7 na
2.7 kwa mtiririko huo wakati ambapo katika majengo ya HIP na Ubungo
Plaza kulikuwa na ongezeko la eneo lililopangishwa kwa asilimia 20.9 na
1.3 mtawalia.
Ni dhahiri kuwa, kwa ujumla, kumekuwa na ongezeko la
ushindani katika sekta ya nyumba na majengo kufuatia kuongezeka kwa
ujenzi unaofanywa na mashirika na taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Hali hii ilipelekea baadhi ya wamiliki wa majengo hayo kubuni mbinu
mbalimbali za kibiashara ikiwa ni pamoja na kubadili matumizi ya majengo
hayo na pia kuweka viwango vya kodi ya pango vinavyoendana na hali
halisi ya soko. Kwa kuzingatia takwimu za hapo juu ni wazi kuwa madai
kwamba mkikimkiki wa ukusanyaji kodi ndiyo umekimbiza wapangaji hayana
mashiko.
Madai ya biashara nyingi kufungwa: Kwa upande wa madai ya
biashara nyingi kufungwa katika siku za karibuni, tumefuatilia na kwa
kiasi fulani kuna ukweli. Imebainika kwamba kasi ya wafanyabiashara
kufunga biashara zao imeongezeka kati ya mwezi Agosti na Oktoba 2016.
Mfano Ilala 1,076, Kinondoni 443, Temeke 222 na Arusha 131. Aina ya
biashara nyingi zilizofungwa ni katika sekta ya ujenzi na biashara ya
jumla na rejareja, na chache katika huduma za usafiri.
Hata hivyo,
sababu hasa zilizopelekea biashara hizo kufungwa hazijabainika kutokana
na ugumu wa kupata taarifa kutoka kwa wenye biashara zilizofungwa.
Sababu za mtu kufunga biashara yake zinaweza kuwa nyingi, ikiwemo,
kushindwa kuingiza bidhaa nchini bila kulipa kodi stahiki, kushindwa
kulipa au kulipwa madeni, kubadilisha aina ya biashara, kushindwa
kusimamia biashara, gharama kubwa za uendeshaji, wabia katika biashara
kutoelewana au kutapeliana, kuibuka kwa washindani wa kibiashara wenye
nguvu au huduma bora zaidi n.k.
4.3 VAT Imekimbiza Watalii
Takwimu
rasmi kuhusu wageni walioingia nchini katika mwaka 2016 kwa ujumla
zinaonyesha kuwa idadi ya wageni imeongezeka ikilinganishwa na mwaka
2015 (Jedwali 4). Hivyo madai kuwa watalii wameikimbia Tanzania kwa
sababu ya VAT kwenye baadhi ya huduma za utalii hayana msingi! Na kama
nia ni kutolipa kodi na wakati huohuo Serikali inadaiwa fedha kwa ajili
ya kuboresha miundombinu ya utalii na huduma nyingine kwa wananchi, hilo
halikubaliki! Nawaalika wadau wa sekta ya utalii waje wajenge hoja
zenye mashiko wakati wa mapitio ya marekebisho ya kodi kwa ajili ya
bajeti ya 2017/18.
Jedwali 4a: Idadi ya Wageni walioingia Nchini 2015 – 2016
Mwezi | 2015 | 2016 | Badiliko % |
Januari | 98,710 | 99,763 | 1 |
Februari | 88,939 | 91,519 | 3 |
March | 77,841 | 93,096 | 20 |
Robo ya Kwanza | 265,490 | 284,378 | 7 |
Aprili | 67,447 | 76,679 | 14 |
Mei | 81,538 | 76,155 | -7 |
Juni | 90,236 | 89,626 | -1 |
Robo ya Pili | 239,221 | 242,460 | 1 |
Julai | 91,896 | 126,755 | 38 |
Agosti | 142,885 | 121,321 | -15 |
Septemba | 100,829 | 121,279 | 20 |
Robo ya Tatu | 335,610 | 369,355 | 10 |
Octoba | 84,121 | 124,623 | 48 |
Jedwali 4b: Idadi ya Wageni waliongia nchini kupitia njia mbalimbali ;
Januari – Septemba
KITUO | 2015 | 2016 | Badiliko % |
JNIA | 238,423 | 252,524 | 5.91 |
KIA | 126,286 | 137,024 | 8.50 |
ZIA | 109,738 | 139,284 | 26.92 |
Namanga | 105,883 | 81,073 | (23.43) |
Kasumulo | 9,871 | 12,006 | 21.63 |
Sirari | 18,899 | 24,393 | 29.07 |
Zanz. Port | 31,994 | 43,242 | 35.16 |
Kabanga | 13,565 | 16,751 | 23.49 |
Manyovu | 17,761 | 18,550 | 4.44 |
- MWELEKEO NA MATARAJIO HADI JUNI 2017
Kwa kuzingatia mwenendo wa ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha
Januari hadi September 2016, matarajio ni kwamba kasi ya ukuaji wa
uchumi kwa mwaka 2016/17 unatarajiwa kufikia asilimia 7.2 kama
ilivyokadiriwa awali.
Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubaki kwenye tarakimu moja.
Thamani
ya shilingi inategemea kuendelea kuimarika kutokana na hatua
zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania.
Kwa upande wa mapato, Serikali inakusudia kufanya yafuatayo hususan katika kuongeza mapato ili kuweza kufikia lengo:
- Kusimamia dhana ya kulipa kodi kwa hiari kupitia udhibiti wa matumizi ya mfumo wa EFDs;
- Kuendelea kuboresha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi hasa yale yanayotokana na michango ya mashirika na wakala za Serikali;
- Kuendelea na majadiliano baina ya serikali na wahisani ili kuhakikisha kwamba fedha za misaada na mikopo zinapatikana kama ilivyopangwa;
- Kuendelea kufanya uthamini wa mkupuo wa majengo ili kukusanya zaidi katika kodi ya majengo;
- Kuendelea kuboresha na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa maduhuli; na
- Kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya kielektroniki. Aidha, MDAs zinahimizwa kutumia mabenki katika kulipia maduhuli.
Aidha, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kusimamia matumizi kama ifuatavyo:-
(i)
Kuendelea kusisitiza nidhamu katika utekelezaji wa bajeti kama
ilivyoidhinishwa kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti ya mwaka
2015;
(ii) Kuendelea kuwianisha mapato na matumizi kwa
kuhakikisha kuwa mgawo wa fedha utaendana na upatikanaji wa
mapato;
(iii) Kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama kupunguza
safari za nje zisizo na tija, matumizi katika sherehe za kitaifa
pamoja na makongamano.
- HITIMISHO
Ninapohitimisha maelezo yangu naomba kusisitiza yafuatayo:
Kwanza:
napenda kuwahakikishia wafanyabiashara kuwa Serikali ya awamu ya Tano
inathamini sana mchango wa Wafanyabiashara katika Maendeleo ya nchi
yetu. Milango ya serikali ipo wazi kwa wale wote wenye hoja zenye
maslahi kwa Taifa letu.
Wizara ya Fedha na Mipango imekwisha toa tangazo
kwa Watanzania na wadau wote wa kodi kuwasilisha mapendekezo ya
marekebisho ya kodi kwa ajili ya uchambuzi na kufikiriwa kuingizwa
katika mapendekezo ya mabadiliko ya kodi katika bajeti ijayo. Ninawaomba
wadau wote kuitumia vizuri fursa hiyo ili tupate mapendekezo mazuri ya
kuboresha mfumo wetu wa kodi na kutupatia mapato zaidi ya kuendeleza
nchi yetu.
Pili: Napenda kutoa rai kwa Watanzania wenzangu
kuhakikisha kuwa tunadai risiti za EFD kila tunaponunua bidhaa au huduma
kama Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania alivyokwisha kuagiza. Yeyote asiyetoa risiti na asiyedai
risiti ajue anatenda kosa na anasaliti jitihada zetu za kuijenga
Tanzania mpya.
Aidha, ningependa kusisitiza kwa wale wote wenye mashine
za EFD wazitumie ipasavyo kwa kila muamala wanaoufanya. Kuna tabia
ambayo imezuka ya kusingizia kuwa mashine imeharibika au kutoa risiti ya
EFD kwa mteja anayeidai tu.
Wale wote wenye tabia hii wanahujumu
maendeleo ya nchi yetu na ninawataka waache mara moja! Nimewaagiza TRA
kufanya kaguzi za kushtukiza na kuwashughulikia ipasavyo wale wasiotaka
kutii maelekezo ya Serikali kwa mujibu wa sheria za nchi.
Napenda
nisisitize kuwa Tanzania mpya ambayo wote tunaitamani iko mikononi
mwetu! Lakini ili tufike huko lazima tufanye kazi kwelikweli – iwe ni
kazi ya kuajiriwa au kujiajiri katika kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara
au huduma au kumiliki viwanda (vidogo, vya kati na vikubwa)!!
Aidha,
lazima kila mmoja wetu alipe kodi stahiki kwa ajili ya maendeleo ya
Tanzania yetu! Tuitikie wito wa Rais wetu kwa vitendo ambaye amedhamiria
kujenga Tanzania mpya ili kuwaondoa Watanzania kwenye lindi la
umaskini haraka. Kulipa kodi ndiyo njia ya uhakika ya kuiwezesha
Serikali kutoa huduma bora zaidi (upatikanaji wa maji, elimu, afya,
umeme, barabara, ulinzi & usalama) kwa wananchi wake.
Uamuzi huu
unahitaji kuachana na mazoea, kujitoa (sacrifice) na kufanya kazi kwa
bidii, nidhamu na uadilifu. Tunataka uchumi ambao wananchi wengi
wananufaika nao, uchumi ambao utajengwa kwa kufanya kazi siyo uchumi wa
ujanja ujanja (mission town), kukwepa kodi au wizi wa mali na fedha za umma.
Tatu:
Wanahabari kwa ujumla mnafanya kazi nzuri sana. Nawaomba mwendelee
hivyo na hasa nikiwasihi mtumie weledi na mjielekeze kuwajuza Watanzania
kuhusu mifano mizuri ya maendeleo hapa nchini na hata katika nchi
nyingine lakini wakati huo huo mtangulize maslahi ya Taifa letu kwanza.
Hata hivyo, yapo magazeti fulani ambayo consistently yanajielekeza kutoa
taarifa za kupotosha na kuifanya jamii ihamaki! Nawaomba: Epukeni kuwa
vipaaza sauti vya nyimbo za watu wachache wenye maslahi binafsi (wawe
wanasiasa, wafanyabiashara, au wafanyakazi) waliozoea “upigaji”!
Punguzeni uandishi wa kuuza magazeti (sensationalism) na uchambuzi wa
mambo kijuujuu! Pimeni taarifa mnazoziandika ili msiwanufaishe
washindani wa nchi yetu kiuchumi (kibiashara au kiuwekezaji) au kuchafua
sura nzuri ya Tanzania!!
Nimalizie kwa kuwahakikishia Watanzania
wote kwamba madai ya baadhi ya magazeti siku za karibuni kuwa uchumi wa
Taifa una hali mbaya siyo ya kweli. Hata gazeti moja la leo limeandika
kuwa “Ripoti ya Uchumi Yashtua”!! Ukweli ni kuwa kama Taifa tumeendelea
kupiga hatua nzuri katika maeneo mengi ya uchumi japo yapo maeneo
machache ambayo yana changamoto, na Serikali inaendelea kuyafuatilia kwa
karibu ili kuyatafutia ufumbuzi. Afya ya uchumi wetu bado ni nzuri na
inatarajiwa itaendelea kuwa ya kuridhisha katika mwaka ujao 2017.
NAWATAKIA WOTE HERI YA MWAKA MPYA 2017
UWE KWELI MWAKA WA HAPA KAZI TU!!
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment