WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuwalinda watoto wa
kike na ndiyo maana inasisitiza waachwe wasome hadi wamalize kidato cha
sita.
Alitoa
kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa vijiji
mbalimbali vya wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi ambako anapita
kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo. Waziri
Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Tumesema
mtoto wa kike aachwe asome hadi kidato cha sita, akifika chuo kikuu
atakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yake lakini kwa sasa waacheni watoto
wa kike wasome. Ninyi vijana, mkibainika mmewapa mimba mabinti
wanaosoma, adhabu yake ni miaka 30 jela,” alisema.
Alisema
nia ya Serikali ni kupata watumishi ambao ni wataalamu wa kada tofauti
kama madaktari, wanasheria, mafundi, walimu na hata Wakuu wa Wilaya
ambao ni wanawake.
Aliwaonya
wazazi ambao huwa wanakubali kuongea pembeni (kupewa fedha) na wanaume
waliowapa mimba mabinti zao na kuwaeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria
ilivyo, nao pia wanastahili kupewa adhabu ya kifungo jela.
“Mzazi
ukigundua binti yako ana ujauzito toa taarifa haraka ili mhusika
akamatwe mara moja. Usikubali kuongelea jambo hili pembeni, nawe pia
utawekwa ndani pamoja na huyo mhusika ambaye tayari ni mhalifu,” alisema
na kuongeza:
“Mwanao
akisema anataka kuoa, mzazi inabidi upeleleze kwanza anataka kumuoa
nani. Asije kuwa anamuona binti ambaye bado anasoma. Akisema anaoa na
wewe ukamkubalia tu, ikija kubainika kuwa ni mwanafunzi, wewe na mkeo
mnakwenda jela miaka mitano mara sita,” alisema huku akionyesha ishara
ya kukunja ngumi.
Akiwa
kwenye baadhi ya vijiji, Waziri Mkuu alielezwa kwamba kuna shule ambazo
zina walimu wa kiume watupu na akamtaka Afisa elimu asimamie suala hilo
kwa kuwahamisha baadhi ya walimu kutoka Ruangwa mjini na kuwapeleka
shuke za vijijini.
“Kuna
shule pale Ruangwa mjini zina walimu wamerundika lakini hapa naambiwa
hakuna Mwalimu wa kike hata mmoja. Hili tatizo kwa wanafunzi wa kike.
Wana masuala ambayo hawawezi kuongea na walimu wa kiume, ni lazime awepo
Mwalimu wa kike wa kusikiliza shida zao,” alisema na kumsisitiza afisa
elimu afuatilie tatizo hilo kwenye shule zote.
Mapema,
akitoa taarifa ya mkoa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw.
Godfrey Zambi alisema mkoa huo unakabiliwa na tatizo la utoro mashuleni
kwani wanaoandikishwa darasa la kwanza si wote wanaomaliza darasa la
saba na vivyo kwa wanaoanza kidato cha kwanza na kumaliza kidato cha
nne.
“Takwimu
zinaonesha mkoa wa Lindi unalo tatizo kubwa sana na ambalo tunaendelea
kulipa uzito wa pekee la kudhibiti wanafunzi wanaoandikishwa kuanza
shule lakini wanashindwa kukamilisha kipindi chao cha miaka saba
shuleni. Idadi kubwa ya wanafunzi ni watoro,” alisema.
Takwimu
za kidato cha nne zinaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa wa shule
walikuwa 4,764 (wavulana 2411 na wasichana 2,353) na watahiniwa wa
kujitegemea walisajiliwa 335 na kati yao watahiniwa 290 (asilimia 86.6)
walifanya mtihani na watahiniwa 45 ambao ni sawa na asilimia 13.4
hawakufanya mtihani.
Kwa
upande wa masomo ya sayansi, shule zilizofanya mitihani ya sayansi ya
vitendo (actual practical) zilikuwa ni 78 (Kilwa 19, Liwale 11, Lindi
Manispaa 9, Ruangwa 4, Lindi vijijini 14 na Nachingwea 21) watahiniwa
ambao hawakufanya mtihani baada ya kusajiliwa ni 100 (wavulana 50
wasichana 50).
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment