Na Nathaniel Limu, Singida
Watu
wawili wakazi wa jimbo la Singida Kaskazini mkoani Singida, wamefariki
dunia baada ya kuugua ugonjwa hatari wa Kipindupindu unaotokana na
uchafu.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi jana ofisini kwake, Mkuu wa wilaya ya
Singida, Elias Tarimo, alisema Novemba, 26 mwaka huu, ugonjwa huo wa
Kipundupindu ulibainika katika vijiji vya Merya na Msange jimbo la
Singida kaskazini.
Hata
hivyo, alisema kuwa ilichukua muda mrefu mno mamlaka zinazohusika kutoa
taarifa ya ugonjwa huo, kitendo kilichochangia idadi ya wagonjwa
kuongezeka na kufikia 30.
“Urasimu
huu umesababisha hatua stahiki za kudhibiti ugonjwa huu, kuchelewa
kuchukuliwa na hivyo kuchangia wananchi wawili kupoteza maisha. Kwa sasa
tumebakiwa na wagonjwa sita kambi ya Merya na Msange wapo watatu,” alisema Tarimo.
Mkuu
huyo wa wilaya, alisema baada ya kupata taarifa hizo kwa kuchelewa,
hawakulala walipiga kampeni ya nguvu kuhimiza usafi wa mazingira,
matumizi bora ya vyoo na kuchemsha maji kwa ajili ya matumizi ya
nyumbani.
“Aidha,
wataalam walipima maji ya visima 14 yanayotumiwa na wananchi wa vijiji
hivyo, na 12 kubainika vina vidudu vinavyochangia ugonjwa wa kipindu
pindu. Baada ya kugundua hivyo, tumepiga marufuku maji ya visima hivyo
kutumika,” alisema.
Akifafanua,
alisema wamewaelekeza wananchi kutumia maji ya bomba na wamechukua
mashine kubwa ya kupampu maji kutoka kijiji cha Sagara.
“Mashine
hii tumeisimika na itasambaza maji ya bomba katika vijiji hivyo vya
Msange na Merya. Hatujaishia hapo, tunaendelea kuwahimiza wananchi
kutumia vidoge vya waterguird kwa ajili ya kutibu maji yawe safi na
salama. Vile vile tanawahimiza kutumia vyoo na kuacha tabia ya
kujisaidia ovyo kwenye vichaka,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Tarimo alisema kuwa baada ya kufanya kampeni ya kuhimza
usafi, mwananchi yoyote atakayeugua Kipindupindu, atatibiwa na akipona,
mara moja atafikishwa mahakamani, kujibu tuhuma ya kutaka kujiuawa kwa
makusudi.
Wakati
huo huo, katika kuchukua hatua kudhibiti Kipindupindu, Manispaa ya
Singida imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo ya kupiga marufuku
wafanyabiashara wa matunda, kumenya matunda. Imeagizwa kuwa matunda yote
yaliwe nyumbani baada ya kuoshwa vizuri kwa maji.
Pia kila kaya imeagizwa kutumia vyoo bora na kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kula chakula na baada ya kutoka chooni.
Mkurugenzi
wa manispaa hiyo, Bravo Kizito Lyapembile, amesema mtu ye yote
akikamatwa kwa kuchafua mazingira, atatozwa faini kati ya shilingi
30,000 na 300,000.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment