WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku watu binafsi wenye uwezo kifedha
kutumia Jeshi la Polisi kuwapiga mabomu na kuwanyanyasa wananchi kwa
kuwapiga mabomu wananchi wasio na silaha.
Ameagiza nguvu hizo wazitumie kwenye maeneo ambayo yanahatarisha usalama wa nchi na wananchi.
Aidha
amewaambia wananchi wa Kata ya Bwawani Kitongoji cha Omapinu kuwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi atafika
kijijini hapo wiki ijayo, kuzungumza nao namna ya kutatua mgogoro wa
shamba la Tanzania Plantation na wananchi hao.
Waziri
Mkuu Majaliwa aliyasema hayo baada ya kusimamishwa na wananchi wa
kitongoji hicho, wakati alipokuwa akiendelea na ziara yake mkoani Arusha
jana.
“Kuanzia
sasa ni marufuku kwa watu binafsi wenye uwezo wa fedha kutumia Jeshi la
Polisi kuwapiga mabomu na kuwanyanyasa wananchi kwa kuwapiga mabomu
wakati hawana silaha.
“Polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu hizo kwenye maeneo ambayo yanahatarisha usalama wa nchi na wananchi na si vinginevyo,” alisema Waziri Mkuu.
Kuhusu mgogoro wa shamba la Tanzania Plantation, Waziri Mkuu alihoji; “Ni
kwanini polisi wawapige mabomu wananchi wanaozuiwa kulima au kuchota
maji katika eneo hilo la shamba hadi kufikia hatua ya wanawake kuharibu
mimba?
“Nyie
polisi kwanini mnawapiga mabomu hawa watu, nani anatoa amri ya kupigwa
mabomu wananchi hawa. Nasema kuanzia leo msiwapige mabomu watu hawa na
pia nawasihi nyie wananchi msifanye fujo, subirini Waziri Lukuvi anakuja
wiki ijayo kwa ajili ya kutatua mgogoro huu wa shamba.”
Alisema
polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu, pale tu panapotokea jambo linaloweza
kuhatarisha maisha au vurugu, ila si kuwanyanyasa wananchi wanaodai
ardhi yao kwa kuwapiga mabomu.
Alisema
Lukuvi atafika mkoani humo kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya
ardhi, ambayo ipo zaidi wilayani Arumeru, na atakaa muda mwingi kwa
ajili ya kutatua kero za wananchi.
Alisema
kuanzia sasa mwekezaji ambaye ana mashamba wilayani humo na
hayaendelezi, mashamba hayo yatachukuliwa na serikali ili kugawanywa kwa
wananchi.
Alisema
Waziri Lukuvi akiwa wilayani humo pamoja na kushughulikia migogoro
mingine, pia atatatua mgogoro huo baina ya shamba la Tanzania Plantation
na wanachi hao.
Awali,
Ofisa Ardhi Wilaya ya Arumeru, Rehema Jato alikiri kuwepo kwa mgogoro
wa ardhi kati ya mwekezaji wa wa Shamba la Tanzana Plantation, Pradeep
Lodhia na wananchi.
Alisema kuna kesi mahakamani na wanachosubiri sasa ni uamuzi wa Mahakama ndipo hatua zingine zichukuliwe.
Mkuu
wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti alisema wilaya hiyo ni moja ya
wilaya nchini zenye migogoro mingi ya ardhi na wakati mwingine watu
wanauana.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment