MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi
(GRC), Anthony Lusekelo maarufu kwa jina la Mzee wa Upako, amewajia juu
na kuwaita wapumbavu, manabii na wachungaji waliompigia simu kumpa pole
baada ya kudaiwa kutishia kuua walinzi wa jirani yake na taarifa hizo
kuandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari.
Mzee wa Upako ameyatoa maneno hayo leo
wakati wa Ibada ya Jumapili katika kanisa lake hilo lililopo Ubungo –
Kibangu jijini Dar huku waumini wake wakiwa na shauku ya kujua
kilichotokea lakini hakuingia kwa undani zaidi ya kutupa lawama kwa
maadui zake.
“Mwaka huu niliahidi kusamehe wote hivyo
nimewasamehe. Kama siaminiki mimi basi iaminini kazi yangu, hakuna
nabii ambaye hajapitia haya ninayopitia.
“Nawaambia manabii na wachungaji
walionipigia simu kunipa pole ni wapumbavu. Ukiwa bondia, basi ukubali
manundu,” amesema Mzee wa Upako akiwa madhabauni hapo na kusema kwa
kifupi kilichotokea:
“Kilichotokea mimi nilikuwa narudi
nyumbani kwangu majira ya saa 10 jioni, nikakutana na vijana wawili, wa
kiume na kike, nikaanza kuwauliza maana ninakoishi ni kama tunaishi
mashetani, sina jirani, kila mtu ana maisha yake, utasikia tu sauti ya
geti asubuhi mtu anatoka na jioni anarudi.
“Sina jirani, hivyo nikawauliza wale
vijana mnakwenda wapi maana tunakoishi hakuna watu wengi na wengi wana
magari yao. Nilikuwa nina haki ya kuwauliza kwani hata ile barabara
nimejenga mimi mwenyewe. Ni kama walikuwa wametumwa vile, cha ajabu
wakaanza kunitukana na mimi kama mwanadamu nilishikwa na hasira,
wakakimbilia kwa jirani ambaye ni mzungu. Lakini yaliyoandikwa wanajua
wenyewe, sisi tufanye kazi ya Injili.
“Vijana wa Kamanda Sirro (Kanda Maalum
ya Dar es Salaam) wananishika na kudhalilisha lakini sitishiki wala
sikati tamaa ilimradi sina sina kosa hata Yesu alishikwa. Kama kuna mtu
anamfahamu nabii au mtume ambaye hajapitia majaribu ambayo mimi
nayapitia anitajie.
“Nimepokea simu nyingi sana za manabii
na wachungaji, ooooh! Mzee wa Upako imekuwaje, nikawatukana pumbavu
maana ni tusi la neno katika Biblia. Nimegundua kwamba kumbe nakubalika,
haijalishi ni kwa mabaya au mazuri, magazeti, tv na media kwa jumla
nimewekwa front page. Kumbe ninauza. Lakini kwa nini hawaandiki mazuri
ninayofanya kama mwanamke niliyemuahidi mtoto ndani ya mwaka huu na
amepata mtoto. Kwa mwaka huu hiliahidi kusamehe hivyo nimewasamehe
wote.”
Mchungaji huyo amesema hatazungumza kwa
undani kama ambavyo wengi walidhani lakini amewaomba waumini wake
wasubiri baada ya mwezi mmoja kuisha.
Akihubiri wakati wa ibada hiyo, Mzee wa
Upako amewasifu waumini wake kwa kufurika kanisani kuliko siku nyingine
yoyote tangu mwaka huu umeanza.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment