Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Katrina Revocati amewataka mahakimu
nchini kuzingatia sheria katika utendaji wao wa kazi hasa katika utoaji
wa dhamana.
Kauli
ya Msajili imekuja wakati kukiwa na malalamiko dhidi ya baadhi ya
mahakimu kuwanyima dhamana washtakiwa ilhali mashtaka yao yanaruhusu.
Aidha,
kauli ya msajili huyo mkuu imekuja wakati mawakili wa Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema wakipambana ili mteja wao apate dhamana baada ya
kukwaa kisiki katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Mashtaka
ambayo kwa mujibu wa sheria dhamana zake zimezuiwa ni ya mauaji ya
kukusudia, uhaini, utakatishaji wa fedha, wizi wa kutumia silaha,
usafirishaji binadamu na dawa za kulevya.
Hata
hivyo, Mahakama inaweza kuzuia dhamana endapo kutakuwa na pingamizi la
kisheria, na mara nyingi mapingamizi hayo yamekuwa yakiambatana na hati
kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Msajili
huyo alitoa maagizo hayo jana mjini Moshi alipokuwa akizungumza na
mahakimu wa ngazi zote katika mahakama za mjini Moshi baada ya kumaliza
ziara ya kikazi katika mkoa wa Kilimanjaro.
Taarifa
iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Bernard
Mpepo ilisema msajili huyo waliwataka mahakimu watunze maadili yao ili
kujenga imani kwa jamii.
Msajili
mkuu pia alitembelea Gereza Kuu la Karanga mjini Moshi na kufanya
ukaguzi wa kawaida na kisha kuzungumza na wafungwa, mahabusi na
wafanyakazi wa gereza.
Akiwa
katika gereza hilo, msajili mkuu alisema mkakati wa Mahakama ni kuona
wateja wanapata huduma bora na ya haraka na tayari mahakimu wamepewa
malengo ya kumaliza kesi haraka.
Ili
kuboresha huduma, alisema mwaka 2017 wamekubaliana katika mahakama ya
mwanzo, shauri lolote lisikae zaidi ya miezi sita wakati mahakama ya
wilaya na mkoa shauri lisikae zaidi ya miezi 12.
Pia
mahakama imeingia mkataba na Shirika la Posta kusambaza nakala za
hukumu kwa wateja na nakala ya hukumu itakuwa inamfikia mdau ndani ya
siku 21.
Chini ya mkakati huo, nakala ya mwenendo wa shauri utamfikia mteja wa mahakama ndani ya siku 21.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment