WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa miezi sita ya kujitathimini mashirika
yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanayofanya kazi zake wilayani Ngorongoro
mkoani Arusha, kama yanafanya kazi kwa misingi ya sheria na maadili.
Baadaye, yatahakikiwa na kama yatabainika yanachochea migogoro, yatafutwa.
Pia,
Majaliwa amezicharukia NGOs nyingine zinazoitangaza vibaya Tanzania
kimataifa kwa kupiga picha za kudhalilisha watoto wakiwa wanatembea
kwenye mawe huku wamevaa kandambili kubwa, kuonesha nchi ni masikini.
Ametaka NGOs hizo kuondoka nchini, la sivyo serikali itazishughulikia.
“Hizi
NGOs zingine si muondoke, nendeni kwingine mkafanye kazi. Halafu nyie
mnaotuma picha za kudhalilisha watoto wakiwa wamevaa kandambili kubwa,
kudai nchi za nje eti Tanzania ni masikini, tutawashughulikia,” alisema
Majaliwa alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ngorongoro jana.
Aidha
alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atakuja
wilayani hapo kukagua kazi walizozifanya, wanazozifanya na miradi
wanaosaidia jamii.
Majaliwa
aliwaambia watumishi hao wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro pamoja
na wadau mbalimbali wakiwemo wakurugenzi wa mashirika yasiyo ya
serikali, yanayofanya shughuli zake wilayani hapo, kuwa serikali haitaki
mashirika chochezi wa migogoro na itayafuta.
Alisema
serikali haitasita kuyafuta mashirika yanayofanya kazi wilayani humo,
ambayo yapo kwa nia ya uchochezi na kuacha kufanya kazi katika malengo
yaliyokusudiwa.
Waziri Mkuu alisema wilaya hiyo, ina mashirika yasiyo ya serikali 30 ambayo yamesajiliwa, lakini yanayofanya kazi ni 19 tu.
Alisisitiza kuwa haiwezekani serikali isajili mashirika hayo, lakini utendaji kazi wake uwe hafifu.
Alisema
ukifuatilia, mashirika hayo utagundua kuwa yanapokea fedha nyingi,
lakini hakuna cha maana wanachokifanya kwa wananchi. Alisema serikali
ina taarifa ya NGOs hizo zinazopewa fedha na wafadhili.
“Najua
taarifa zenu mnapokea kiasi gani cha fedha na mnazifanyia nini, lakini
namleta Mkaguzi wa serikali ili akague mnatumiaje fedha zenu, nawapa
miezi sita tu halafu ukaguzi utaanza, maana kuna mashirika mengi lakini
kazi mnazofanya hazionekani,” alisema Majaliwa.
Alisema
baadhi ya mashirika, yana akaunti nchi jirani ya Kenya na mengine kama
PWC anapewa Sh bilioni 2.5 kwa mwaka na shirika la UCRT linapokea Sh
bilioni 1.5 kwa mwaka, lakini hajui yanafanya nini.
“Nina
taarifa zenu mnapata hela nyingi, lakini mnahudumia vipi jamii hakuna,
sasa ngojeni ukaguzi ufanyike halafu nitachukua maamuzi maana kila siku
Loliondo kuna nini hapa mnasajiliwa halafu hakuna cha maana,” alisema.
“Kuna
nini Loliondo, kwani kila mara Loliondo nina taarifa za kila NGOs
zinazofanya kazi hapa, najua mnachokifanya, sasa nawaambia serikali
haitawafumbia macho kuona hiki ninachokifanya hapa na ikigundulika
mnafanya kinyume na matakwa ya usajili tutazifuta”.
Alisema
serikali itazifuta NGOs zote, ambazo zitabainika ni kiini cha migogoro
Loliondo. Alitoa hadhari kwa kampuni zinazofanya kazi zake bila usajili,
kuwa zikigundulika, zitachukuliwa hatua.
Aliwageukia
watumishi wa umma na kuwatahadharisha wale wanaotoa taarifa za migogoro
ya ndani kwa wahusika wa NGOs na kisha kuzituma nje ya nchi kwenye
mitandao ya kijamii na barua pepe.
Alisema kuwa nao watashugulikiwa, kwa kuwa wanapaswa kuwa majibu ya migogoro na si wasambazaji wa habari mbaya za nchi.
Alisisitiza
watekeleze kikamilifu kauli ya ‘Hapa Kazi Tu’ ; na si kutumia NGOs kwa
ajili ya kudai kuwasaidia wananchi, huku wakijua kuwa wananchi
hawanufaiki na fedha hizo wanazopewa na wafadhili Awali akizungumza na
watumishi wa halmashauri ya Wilaya hiyo, Majaliwa alitoa tahadhari kwa
madiwani kuacha kushirikiana na watu wa Uhasibu wanaotoa hela kwaajili
ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema baadhi ya madiwani, wanakwamisha miradi ya maendeleo kwa kula fedha kwa sababu ya ukaribu walionao.
Akizungumzia
nidhamu ya fedha, Majaliwa alisisitiza kila mtumishi lazima afanye kazi
kwa bidii, ikiwemo kutoa huduma bila kuwabagua wananchi kwa itikadi zao
za vyama.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment