Katika maisha ya
kimapenzi hakuna kitu kinachouma kama kusalitiwa, tena kusalitiwa
kunakouma zaidi ni pale unapobaini mpenzi wako kampa penzi mtu
unayemjua halafu ukijilinganisha wewe na huyo aliyepewa unashindwa
kuelewa kilichomshawishi mpenzi wako.Lakini
licha ya kwamba usaliti si kitu kizuri, watu wamekuwa wakisalitiana,
tena sana tu. Inafika wakati unashindwa kuamini kama yupo mtu ambaye
hajawahi kumsaliti mpenzi wake.Niseme
tu kwamba wapo wachache waliotulia ila asilimia kubwa ya walio kwenye
uhusiano ni wasaliti hata tafiti zimethibitisha hilo. Kama hali yenyewe
iko hivyo, cha kujiuliza ni kwamba unapobaini mpenzi wako kakusaliti
ni kipi unachotakiwa kufanya? Je, ni kuamua kunywa sumu kama ambavyo
wamekuwa wakifanya wengine? Sidhani kama huo ni uamuzi sahihi. Mtaalam
wa masuala ya mapenzi James Johnson kutoka Marekani amependekeza mambo
10 unayoweza kufanya baada ya kubaini kuwa mpenzi wako amekusaliti.1. Kubaliana na kilichotokea
Kama
kishakusaliti ni tukio ambao limeshatokea na haliwezi kufutika. Kubali
kuwa umetendwa, huzunika lakini mwisho liache lipite ili uweze
kujipanga upya.
2. Usijilaumu
Wapo ambao wakishasalitiwa
hujuta kukubali kuingia kwenye uhusiano na watu waliowatenda. Utamsikia
mtu akisema ‘najuta kumkubalia awe mpenzi wangu’. Kujilaumu kwa namna
hiyo hukutakiwi kwani kutakufanya uzidi kunyong’onyea.
3. Jitoe
Jifanye
kama vile aliyesalitiwa siyo wewe bali ni rafiki yako kisha jiulize
ungemshaurije? Ushauri ambao ungempata basi uchukue kisha uufanyie kazi.
4. Pima ulivyoathirika
Je,
kitendo cha mpenzi wako kukusaliti kimekukosesha imani juu yake? Kama
ni hivyo, unadhani una sababu ya kuendelea kuwa naye au unahisi madhara
aliyokupatia huwezi kumvumilia?
5. Mpasulie ukweli
Kwa
vyovyote utakavyoamua ni lazima umweleze juu namna alivyokuumiza kwa
usaliti wake. Hata kama utampa nafasi nyingine lazima ajue jinsi
alivyokuumiza ili iwe changamoto kwake.
6. Chunguza kwa nini kakusaliti
Usiliache
likapita hivi hivi, unatakiwa kujua sababu ya yeye kukusaliti. Je,
kuna ambacho anakikosa kwako au ni tamaa zake tu? Jibu utakalolipata
litakusaidia katika maisha yako ya kimapenzi.
7. Usikubali akulainishe
Huenda
huyo mpenzi wako ni ‘msanii’ na anaweza kukulainisha kwa maneno ambayo
yanaweza kukufanya ukalichukulia tukio hilo kiurahisi. Kuwa na msimamo
na eleza hisia zako kwa uwazi.
8. Amua kusuka au kunyoa
Likishatokea
hilo jaribu kuzungumza na moyo wako. Uamuzi wa kuendelea kuwa naye au
kumuacha uuchukue bila shinikizo. Hata kama kakuumiza, kama unadhani
unaweza kumpa nafasi nyingine mpe ili usije ukajuta baadaye kwa kumkosa
lakini kama unaona moyo wako unamkataa, muache.
9. Msamehe
Kwa
uamuzi wowote utakaochukua ni lazima uwe tayari kumsamehe ili
kuliondoa dukuduku lako rohoni. Kutokumsamehe kunaweza kukufanya ukawa
unaumia kila wakati na kukosa amani.
10. Iwe fundisho kwako
Chukulia
tukio hilo kama fundisho kwako. Huenda wewe ndiye uliyechangia
kusalitiwa, kama ni hivyo badilika ili yasije yakakukuta kama hayo
utakapokuwa na mwingine. Pia kama kusalitiwa kumetokana na kutoridhika
kwa mpenzi wako, kuwa makini wakati wa kuchagua mwingine wa kuwa naye.
Post a Comment