Na Benny Mwaipaja-WFM, Dar es salaam
Benki
ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti
nafuu wa dola Milioni 164, karibu Shilingi Bilioni 360, kwaajili ya
kuchangia Bajeti kuu ya Serikali katika kipindi cha Mwaka wa Fedha
2016/2017 pamoja na kuongeza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo
nchini-TADB.
Mikataba
miwili imesainiwa jana Jijini Dar es salaam kati ya Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James kwa niaba ya Serikali na
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeondoka Dkt. Tonia
Kandielo.
Mkataba
wa kwanza uliosainiwa ni kwa ajili ya kutunisha Mfuko Mkuu wa Serikali
ambapo Benki hiyo imetoa dola za kimarekani milioni 70 sawa na tsh 154
bilioni ambazo zitaelekezwa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Shirika
la Ugavi wa Umeme nchini-TANESCO.
Mkataba
wa pili ni kwaajili ya kuongezea mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo
nchini-TADB wenye thamani ya dola Milioni 94 sawa na shilingi Bilioni
204 kwa ajili ya kuiongezea uwezo Benki hiyo kutoa mikopo yenye riba
nafuu kwa wakulima ili kuongeza mnyonyoro wa thamani kuanzia uzalishaji,
uongezaji thamani na upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya
wakulima.
Uhai
wa mikopo yote miwili utakuwa ni miaka 40 ambapo serikali itaanza
kuilipa baada ya miaka kumi tangu kutolewa kwake, huku riba yake ikiwa
chini ya asilimia 1.
Akizungumza
baada ya kusainiwa kwa mkopo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James, amesema mkopo huo umekuja wakati muafaka na
utasaidia kukuza na kuimarisha TANESCO na kuendeleza kilimo nchini.
“Tanzania
ni nchi iliyonufaika zaidi na mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki
ya Maendeleo ya Afrika-AFDB ikilinganishwa na nchi nyingine yoyote
iliyoko katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika,” alisema Bw. James.
Kwa
upande wake, Mwakilishi Mkazi wa AFDB anayeondoka Dkt. Tonia Kandielo
amesema kuwa hadi sasa Benki yake imeipatia Tanzania mkopo wenye thamani
ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2, ambazo zimewekezwa kwenye
miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji,
nishati ya umeme, elimu na kilimo.
“Ninaamini
kuwa hatua ya kuongeza mtaji katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo-TADB
itachochea maendeleo ya kilimo nchini, na tunaahidi kuwa tutaendelea
kuiwezesha zaidi siku zijazo,” alisema Dkt. Kandielo.
Kuhusu
Sekta ya Nishati, Dkt. Kandielo amesema kuwa Benki yake imeona umuhimu
wa kuliwezesha shirika hilo ili liweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi
ili kuchochea uchumi wa Taifa.
“Mikopo
hii inahusiana na vipaumbele tulivyoviweka kama Benki ambavyo viko
katika malengo matano ambapo tunataka kuwekeza katika sekta ya nishati,
uzalishaji wa chakula, kuendeleza viwanda, kuiunganisha Afrika na
kuboresha maisha ya waafrika kwa ujumla,” aliongeza Dkt. Kandielo
Wakati
huo huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amemuaga rasmi
Dkt. Tonio Kandielo ambaye amehamishiwa nchini Afrika Kusini kuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo atakaye simamia Kanda ya Kusini mwa
Afrika.
Dkt.
Mpango, amesifu jitihada kubwa zilizofanywa na mwana mama huyo katika
kipindi cha miaka 6 aliyokuwepo hapa nchini ambapo ameweza kusimamia
vizuri maslahi ya Tanzania katika Benki hiyo.
Amesema
kuwa katika kipindi hicho Tanzania imeshuhudia maendeleo makubwa katika
sekta za ujenzi wa miundombinu ya barabara, kilimo, maji na umeme,
ambapo benki hiyo ilihakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa viwango
vinavyotakiwa.
Amemwomba
Mkurugenzi Mkuu huyo kuwezesha upatikanaji wa fedha kwaajili ya ujenzi
wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard gauge) inayohitaji
fedha nyingi, kusimamia utekelezaji wa mradi wa umeme wa kikanda
unaoanzia nchini Zambia, uboreshaji wa Bandari ya Itungi na Mbambabay.
Akijibu
hoja za Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Dkt. Tonia
Kandielo amesema kuwa anaamini mrithi wake ataendeleza mazuri
aliyoyafanya na kwamba yeye binafsi atahakikisha anafuatilia kwa karibu
miradi ambayo mikataba yake imesainiwa katika nyanja za maboresho ya
sekta ya umeme na kilimo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment