BARAZA
la Sanaa la Taifa (Basata), linalosimamia sanaa na burudani nchini,
limeonya wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani, kuepuka kuruhusu
disko toto na kujaza watu kwenye kumbi hizo.
Aidha,
Baraza hilo pia limesisitiza kuwa halitafumbia macho ukumbi utakaokiuka
maelekezo yake, ikiwa ni pamoja na kuruhusu maonesho machafu yenye
kudhalilisha utu hasa yanayoonesha maungo ya ndani, kwa kuwa
yameshapigwa marufuku.
Hayo
yamo kwenye taarifa ya Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, kwa lengo la kuwatakia wasanii
na wadau wote wa sanaa heri ya Krismasi na Mwaka mpya.
Huku
ikisisitiza kauli mbihu yake kuwa ‘Sanaa ni kazi tuikuze, tuilinde na
kuithamini’, Basata iliwataka wamiliki na waendeshaji wa kumbi za
burudani, kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizo kwenye vibali vyao
vya uendeshaji kumbi.
“Wanaelekezwa
kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao,
kuzingatia muda wa matumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye
maeneo maalumu hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa
maisha ya watu na mali zao,” ilieleza taarifa hiyo.
Basata
pia iliwakumbusha wamiliki wa kumbi za sherehe na burudani, kuwa
inakatazwa kukusanya watoto kwenye kumbi hizo kupitia ‘Disko Toto’
katika msimu huu wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, ili kuepuka maafa
yanayoweza kujitokeza.
“Uzoefu
unaonesha, kwamba nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi
hujisahau na kuandaa madisko toto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa
ambayo yangeepukika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
“Aidha,
baadhi ya wamiliki na waendeshaji kumbi wamekuwa wakijisahau na
kuendekeza faida bila kujali maelekezo ya vibali vyao, wamekuwa wakijaza
watu kupita viwango vya madaraja waliyopangiwa na Basata,” ilieleza taarifa hiyo na kuonya kuwa hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekiuka maagizo hayo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
Post a Comment